Mji wa Mbinga ambao hivi sasa unakua kwa kasi. |
Na Muhidin Amri,
Mbinga.
WANANCHI wanaoishi katika mji wa Mbinga mkoani Ruvuma wameiomba
serikali kupitia Wizara ya maji na Umwagiliaji, kuchukua hatua katika mipango yake
kupanua mradi wa maji safi na salama katika mji huo, hatua ambayo itawezesha
wananchi wengi kupata huduma ya maji safi na salama.
Ushauri huo ulitolewa na wananchi hao walipokuwa wakizungumza
na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, kufuatia hivi sasa wamekuwa wakitumia
muda mwingi kwenda umbali mrefu kutafuta huduma ya maji hayo kwa ajili ya
matumizi mbalimbali majumbani kwao.
Walisema kuwa hali hiyo inatokana na miundombinu inayotumika sasa kuchakaa na wakati mwingine huharibika mara kwa mara, jambo ambalo limekuwa
likiwafanya kupata maji kwa mgao na kuwa kero kubwa kwao.
Walifafanua kuwa serikali kupitia Mamlaka ya maji safi na
usafi wa mazingira katika mji wa Mbinga (MBIUWASA) umefika wakati sasa,
kuchukua hatua ya kuipatia ruzuku ya fedha itakayoweza kuifanya mamlaka hiyo
kuboresha miundombinu yake ya maji katika mji huo, ili wananchi waweze
kuondokana na adha wanayoipata sasa.
Dickson Ndunguru ambaye ni mkazi wa Mbinga mjini alisema
kwamba hali ya upatikanaji wa maji katika mji huo hasa kwa kipindi cha kiangazi
imekuwa ni vigumu upatikanaji wake, licha ya ukweli kwamba mji wa Mbinga umezungukwa
na mito na mifereji mingi ambayo hutiririsha maji kipindi cha mwaka mzima.
Kwa upande wake Meneja MBIUWASA Patrick Ndunguru, alipohojiwa
juu ya hali hiyo alisema kuwa kero hiyo ya uzalishaji mdogo wa maji inatokana
na kuchakaa kwa miundombinu ya kuleta na kusambaza maji katika mji huo, kutoka
kwenye chanzo kikuu cha Ndengu kilichopo kijiji cha kihereketi kata ya Nyoni
wilaya ya Mbinga.
“Ni kweli tuna upungufu mkubwa wa maji katika mji wetu, tatizo
hili linachangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa fedha hivyo kama serikali itasaidia
Mamlaka kuipatia fedha za kutosha tutaweza kuboresha miundombinu husika
iweze kuwa ya kisasa zaidi, ambayo itazalisha maji mengi yanayotosheleza
mahitaji ya wakazi wa mji wa Mbinga”, alisema Ndunguru.
No comments:
Post a Comment