Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imepata zawadi
ya shilingi milioni 331,252,720 baada ya kukidhi vigezo vitatu vya utekelezaji wa
shughuli mbalimbali za maendeleo, katika sekta ya elimu wilayani humo.
Vigezo vilivyoifanya halmashauri hiyo iweze kupata tuzo hiyo
ni kupanga walimu katika shule zake kulingana na mahitaji husika, kuandaa takwimu
za shule zote na kuziweka kwenye mtandao pamoja na kutuma fedha za ruzuku ya
uendeshaji kwa wakati kwenye shule husika.
Ofisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Samwel Komba alisema hayo
wakati alipokuwa akisoma taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru
Kitaifa, George Mbijima juu ya mikakati ya kukuza elimu katika shule za msingi
wilayani humo.
Komba alifafanua kuwa fedha hizo wamezipata kutoka kwa
wafadhili wa maendeleo nchi ya Marekani, Uingereza, Sweeden, Benki ya dunia na
shirika la Jica ambao wanatekeleza programu inayojulikana kwa jina la Lipa
kulingana na matokeo kwa kushirikiana na serikali kuu hapa nchini.
Alisema kuwa wamepewa maelekezo juu ya matumizi ya fedha hizo
ambapo ni pamoja na kutenga asilimia tano kwa shughuli za kimaendeleo, kutoa
motisha kwa shule na viongozi wa kata wanaohusika na masuala ya elimu.
Hivyo basi katika kutekeleza hilo halmashauri ya wilaya ya
Mbinga, imenunua pikipiki mbili zenye thamani ya shilingi milioni 4,700,000
ambazo wamepewa Waratibu elimu kata ya Kitura na Matiri wilayani humo.
“Lengo la kuwapatia pikipiki hizi ni kuweza kuwasaidia
kurahisisha kazi za ufuatiliaji shuleni, katika kukuza taaluma na kuboresha
miundombinu husika katika shule zetu hapa wilayani”, alisema Komba.
Pia jumla ya shule nane za msingi na sekondari wilayani humo,
zimepata mgao wa fedha hizo kwa kupewa kila shule shilingi 200,000 kila mmoja
na kufanya jumla ya shilingi milioni 1,600,000.
Shule za msingi za wilaya hiyo ambazo zimepata fedha hizo ni
Kitai, Ilela, Longa, Mbugu, Maguu na kwamba kwa shule za sekondari ni Linda,
Mkumbi na Mipalu zote zilizopo wilayani Mbinga.
Pamoja na mambo mengine, kwa upande wake kiongozi wa mbio
hizo za Mwenge wa uhuru kitaifa, Mbijima alipongeza usimamiaji mzuri unaofanywa katika
sekta ya elimu wilayani Mbinga na kuagiza kwamba, uwe endelevu kwa faida ya
kizazi cha sasa na baadaye.
No comments:
Post a Comment