Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI waishio katika kata ya Kitura wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma, wameulalamikia uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)
mkoani humo kwa kushindwa kufanyia matengenezo kwa muda mrefu barabara ya kutoka
kata ya Litembo hadi kijiji cha Nkili wilayani Nyasa, jambo ambalo limekuwa
likisababisha kero kubwa kwao hasa pale wanaposafirisha wagonjwa au mazao yao
kutoka shambani.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. |
Barabara hiyo ambayo ina zaidi ya kilometa 30 walisema,
kutokana na kuwa katika hali mbaya wamekuwa wakati mwingine wakilazimika
kutumia jembe la mkono kuitengeneza, hasa nyakati za masika magari yao
yanapokuwa yanakwama barabarani.
Malalamiko hayo yalitolewa juzi na wananchi hao, kwenye kikao
cha baraza la kata kilichofanyika kwenye ofisi ya makao makuu ya kata ya Kitura
wilayani Mbinga na kuhudhuriwa na Diwani wa kata hiyo, Alex Ngui ambacho
kililenga kujadili maendeleo ya kata hiyo.
Walifafanua kuwa katika kipindi hicho cha masika, hata
wanaposafirisha wagonjwa wao hulazimika kuwabeba kwenye machela kuwapeleka
hospitali ya Litembo, ambayo ipo jirani na kata hiyo kutokana na magari
kushindwa kupita kufuatia barabara hiyo kuwa katika hali mbaya.
Walieleza kuwa wanamuomba Mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu,
aingilie kati kutatua kero hiyo ili kuweza kunusuru tatizo hilo lisiendelee
kutesa wananchi ukizingatia kwamba, kata hiyo pia ina wakulima wengi ambao
wamekuwa wakizalisha zao la kahawa kwa wingi ambalo limekuwa likiingizia
serikali mapato makubwa.
“Sisi tunaiomba serikali isikilize kilio chetu cha
kutengeneza barabara hii ni miaka mingi imepita hakuna utekelezaji uliofanyika,
tumekuwa tukijitolea kuchimba kwa jembe la mkono ili watu waweze kupita kwa
muda”, walisema.
Kwa upande wake akizungumza katika kikao hicho, Diwani wa
kata ya Kitura Ngui aliongeza kuwa hata barabara ambazo inabidi zihudumiwe na
halmashauri hiyo kwa ajili ya matengenezo ya kila mwaka, zina hali mbaya na ni
kikwazo kikubwa katika usafirishaji wa mazao ya wakulima kutoka shambani kwenda
kwenye masoko.
Hata hivyo Ngui alisema kwamba tatizo hilo atalifikisha kwa
uongozi husika wa wilaya na mkoa, ili liweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu na
wananchi wake waweze kuondokana na kero hiyo ambayo inaendelea kuwatesa kwa
muda mrefu na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi wake.
No comments:
Post a Comment