Na Muhidin Amri,
Songea.
SHIRIKA lisilokuwa la serikali ambalo linahudumia wazee
katika mikoa ya Ruvuma, Iringa na Njombe (PAD) limesema kuwa bado kuna
tatizo kubwa la utekelezaji wa sera za wazee katika mikoa hiyo kutokana na taratibu
husika zilizowekwa kuhudumia watu hao, kutosimamiwa ipasavyo na kufikia hatua
wazee kukosa haki zao za msingi.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, Isihaka Msigwa alisema
hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ambapo ameitaka
jamii kuwapa kipaumbele wazee kila wanapofika katika maeneo ya kutolea huduma
kama vile hospitali na kwenye vyombo vya usafiri, kama vile magari ya
kubeba abiria (daladala).
Msigwa alisema kuwa kukosekana kwa mapango mkakati wa
utekelezaji wa sera ya taifa ya wazee, kumesababisha hata vituo vya kulea
watu hao kuwa vichache na miundombinu yake kutokuwa rafiki kwao.
Alitolea mfano akisema kwamba hadi sasa idadi ya vituo vya
kulelea wazee hapa nchini vipo 20 tu kwa nchi nzima na kwamba, katika masuala
ya ugonjwa wa Ukimwi hayajawekewa sera ya taifa itakayosaidia kundi hilo ambalo
kwa kiasi kikubwa huathirika na ugonjwa huo.
Msigwa ambaye pia ni Katibu mtendaji wa mtandao wa kinga ya jamii
hapa nchini alifafanua kuwa, mapitio mengi ya sera ya Ukimwi mwaka 2010
yameingiza kundi la wazee na kuelekeza namna wazee, watakavyoshughulikiwa lakini
bado inawalenga kuwasaidia hasa watu wa kuanzia miaka 15 hadi 45.
Kwa upande wake pia aliishukuru serikali ya awamu ya tano,
kwa kuunda Wizara itakayohusika na masuala ya wazee ambapo hivi sasa
wameanza kunufaika na matunda ya serikali, kwa kuwekewa chumba maalum cha
matibabu pale wanapokwenda kwenye zahanati, vituo vya afya au hospitali.
Alibainisha kwamba hapo awali kuna baadhi ya vitu vilikuwa
vikisababisha sera ya wazee kushindwa kutekelezeka na kushindwa kupata huduma
zao za msingi, licha ya taifa kutambua kwamba wameitumikia nchi hii katika
mambo mengi ya kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment