Sunday, June 12, 2016

NYASA WALIA NA BAADHI YA VIGOGO WA SERIKALI WALIOPEWA VIWANJA NA KUTOVIENDELEZA KWA MUDA MREFU



Na Muhidin Amri,
Nyasa.

HALMASHAURI ya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, imetakiwa kuongeza kasi ya kupima viwanja katika mji mdogo wa Mbamba bay wilayani humo kutokana na mji huo kukua kwa haraka na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu wanaokwenda huko, kwa lengo la kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuwekeza katika sekta ya uchumi.

Hayo yalisemwa mwishoni wa wiki na baadhi ya wakazi wa mji  wa Mbamba bay, walipokuwa wakizungumzia juu ya ukosefu wa huduma muhimu kama vile hoteli za kisasa na huduma ya usafiri  wa uhakika, kutoka kwenye mji huo na maeneo mengine ya  wilaya jirani ya Mbinga.

Samwel Sogolo na Mariam Majika kwa nyakati tofauti walifafanua kuwa licha ya serikali kuanza kupima viwanja na maeneo ya wazi, kwa ajili ya makazi na shughuli mbalimbali bado kunahitajika kasi kubwa ya upimaji na utambuzi wa maeneo hayo ambapo kufanya hivyo kutasaidia  watu watakaopata viwanja hivyo kuviendeleza kwa kujenga nyumba za kisasa, ikiwemo kuwekeza katika miradi ya  kiuchumi.


Walisema mji huo ni miongoni mwa miji inayokuwa kwa kasi hapa nchini kutokana na uwepo wa bandari ambayo ni kiungo muhimu, kwa nchi  za  nyanda za juu Kusini mwa Afrika ambazo ni Tanzania, Malawi na Msumbiji ambapo watu wake huitumia bandari ya Mbamba bay kwa ajili ya shughuli zao za kila siku.

Kadhalika walieleza kuwa ni rahisi kwa wananchi wa Nyasa, hasa wafanyabiashara kutumia usafiri wa majini kwenda nchi jirani ya Malawi na Msumbiji kufuata bidhaa kutokana na mji wa Mbamba bay, kukosa mahitaji muhimu kwa sababu ya kukosekana kwa wafanyabiashara wakubwa ambao wangeweza kusambaza na kuwekeza katika sekta hiyo muhimu.

Naye Mariam Majika aliongeza kuwa mji huo unasonga mbele kila kukicha hivyo umefika wakati kwa serikali kuwabana watu waliopewa viwanja, kuanza ujenzi wa nyumba za kisasa haraka iwezekanavyo ambazo ujenzi huo utakapokamilika uende sambamba na upatikanaji wa huduma za kijamii.

Alifafanua kuwa kuna watu wengi kutoka nje ya wilaya ya Nyasa, wanaokwenda kwa lengo la kutaka kufanya uwekezaji lakini wanashindwa kufikia malengo yao kutokana na tatizo lililopo la halmashauri ya wilaya hiyo bado halijakamilisha kufanya tathimini maeneo yote husika na hata kwa yale yaliyopimwa, inadaiwa kwamba wamepewa vigogo wachache wa serikali ambao hadi sasa wameshindwa kuyaendeleza.

Majika ameiomba Wizara ya ardhi na maendeleo ya makazi, kuingilia kati  juu ya umiliki wa maeneo hayo ambayo hayaendelezwi kwa muda mrefu wapewe watu wengine wenye uwezo wa kufanya uwekezaji, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadae.

Pia Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Nyasa, Jabir Shekimweri alipoulizwa juu ya madai hayo alisema kwamba hivi sasa wapo katika mkakati wa kuendelea kupima maeneo yote na kulipa fidia watu husika na kwamba yale ambayo tayari wamekwisha pima, wataendelea kuhamasisha wamiliki waliogawiwa ili waweze kuyaendeleza kwa haraka zaidi.  

No comments: