Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, George Mbijima
amewataka viongozi waliopo katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma, kuhakikisha kwamba fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya
kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi, zinafanya kazi iliyolengwa ipasavyo
ili ziweze kuleta tija katika jamii.
Aidha aliagiza kwamba miradi hiyo inapaswa kutekelezwa kwa
wakati, ili kuweza kusaidia kuharakisha mipango mbalimbali ya kimaendeleo
ambayo inalenga kuwaondolea umaskini wananchi.
Mbijima alisema hayo jana alipokuwa kwenye ziara ya mbio za
Mwenge wa uhuru wilayani humo, ambapo jumla ya miradi saba yenye thamani ya
shilingi milioni 701,652,180 Mwenge huo katika miradi hiyo baadhi yake umeweza
kufanya kazi ya kuweka mawe ya msingi, kufunguliwa na kuzinduliwa.
Katika miradi hiyo, nguvu za wananchi ni milioni 71,741,400
mchango wa halmashauri ya wilaya milioni 203,000,000 serikali kuu milioni
52,500,000 na taasisi mbalimbali ni milioni 374,410,780.
“Ni wajibu wenu watumishi wa umma kufanya kazi kwa kufuata
taratibu na miongozo iliyowekwa na serikali, ili tuweze kufikia malengo
tuliyojiwekea na kulifanya taifa letu liweze kusonga mbele kimaendeleo na
wananchi waweze kuondokana na umaskini”, alisema Mbijima.
Vilevile aliwataka watendaji hao wa serikali, kutenga maeneo
kwa ajili ya vijana kufanyia biashara ikiwa ni lengo la kuwafanya waweze kukua
kiuchumi.
Kadhalika alisisitiza kwamba vijana hao, wahamasishwe pia kuunda
vikundi vya ujasiriamali ambavyo vitasajiliwa kisheria na kuweza kuwafanya
waweze kukopesheka na taasisi za kifedha katika kuendeleza shughuli zao za
ujasiriamali.
Pamoja na mambo mengine, kwa mujibu wa risala ya utii wa
wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Magufuli ambayo ilisomwa na Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga
alisema kuwa tathimini ya mwaka 2015 inaonesha kuwa pato la mwananchi wa wilaya
hiyo kwa mwaka, linakadiriwa kuwa ni milioni 2,082,167 ukilinganisha na
shilingi 400,000 kwa mwaka 2007.
Lengo la Halmashauri hiyo alisema ni kuongeza pato hilo la
sasa na kufikia milioni 2,500,000 ifikapo mwaka 2025 kutokana na wananchi wengi,
kuwa na mwitikio mkubwa wa kufanya shughuli za kiuchumi kama vile kilimo cha
mazao ya chakula na biashara.
No comments:
Post a Comment