Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KAYA maskini zilizopo katika kijiji cha Likwera kata Nyoni Halmashauri
ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wameweza kunufaika na mpango wa kunusuru
kaya hizo kwa kupewa fedha shilingi milioni 3,925,000 na Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF) awamu ya tatu, kwa ajili ya kuendeshea miradi ya ufugaji bora wa
kuku, nguruwe na mbuzi.
Husna Chiponda ambaye ni Afisa mtendaji wa kijiji hicho
alisema kuwa jumla ya kaya 91 zimewezeshwa fedha hizo, ambazo wamelipwa kwa
awamu ya mwisho kwa lengo la kuwawezesha waweze kujikwamua kimaisha na
kuondokana na umaskini uliokithiri miongoni mwao.
Aidha aliongeza kuwa kwa upande wa sekta ya elimu, watoto wa
shule za msingi wamenunuliwa mahitaji ya shule na kwamba wa sekondari
wamelipiwa ada na kupewa mahitaji ya aina mbalimbali, kama vile sare za shule, madaftari
na kalamu za kuandikia.
“Watoto 34 wanaosoma sekondari tumewanunulia mahitaji muhimu
na kulipiwa ada, kadhalika kwa shule za msingi wapo 19 nao pia tumewapatia
mahitaji muhimu”, alisema Husna.
Awali alifafanua kuwa
katika awamu iliyopita kaya hizo maskini, ziliwezeshwa shilingi milioni
3,860,000 kutoka pia katika mfuko huo wa TASAF awamu ya tatu katika kijiji hicho
cha Likwera.
Husna aliwataka wananchi hao pia kujenga tabia ya kujitokeza
katika mikutano pindi wanapotakiwa kufanya hivyo, hasa ikizingatiwa kwamba
baadhi yao hata kwenye mkutano wa kuzitambua kaya maskini unapofanyika wamekuwa
hawajitokezi jambo ambalo linasababisha wachaguliwe wasio na sifa.
Alifafanua kuwa kwa wale ambao watajiingiza kwenye mpango huo
wakati wao sio kaya maskini endapo kama watabainika, wataondolewa mara moja na
kwamba aliwaasa wananchi kutoa ushirikiano wa dhati ili mpango huo uweze kufikia
katika mafanikio yaliyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment