Na Mwandishi wetu,
Nyasa.
WAKAZI wanaoishi katika mji mdogo wa Mbamba bay wilaya ya
Nyasa mkoani Ruvuma, wamesema kwamba hivi sasa tangu kuanza kwa mfungo mtukufu
wa mwezi wa Ramadhani wanashindwa kula kitoweo cha samaki, kutokana na
kuuzwa kwa bei ghali tofauti na miezi mingine ya kawaida.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu, baadhi ya
wakazi hao walidai kuwa hali hiyo inatokana na kutoweka kwa samaki katika ziwa
nyasa ambapo hivi sasa hawapatikani kwa urahisi, hivyo wavuvi hutumia
nafasi hiyo kuongeza bei mara dufu zaidi.
Walisema kuwa wilaya ya Nyasa upatikanaji wa mazao mengine ya
jamii ya mboga mboga kama vile maharage, kunde, mbaazi na choroko imekuwa
ni tatizo ambapo watu wengi hutegemea samaki pekee ikiwa ni mboga ya kila
siku katika kuendeshea familia zao.
Hali hiyo walisema wakati mwingine, huwalazimu kutumia mboga
mbadala kama vile kisamvu kutokana na uhaba wa tatizo la upatikanaji wa samaki.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake mmoja wa wakazi wa Mbamba
bay, Said Juma alieleza kuwa mbali na kukumbwa na hali hiyo waumini wa
dini ya Kiislam kuwa na mahitaji makubwa ya bidhaa mbalimbali ikiwemo samaki,
lakini baadhi ya wavuvi wameacha kuendelea na kazi yao ya uvuvi kutokana na
kupanda kwa bei ya leseni ya uvuvi kutoka shilingi 10,000 ya awali hadi kufikia
shilingi 40,000 kwa mtumbwi mmoja, unaotumika kwa kazi hiyo ya uvuvi
wilayani Nyasa.
Juma alifafanua kuwa halmashauri ya wilaya hiyo, inawatoza
kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kulipia leseni ambacho hakilingani na
mapato wanayopata, ambapo alisema hali hiyo inachangia baadhi yao kuachana na
kazi hiyo ambayo wanadai haina maslahi kwao.
Naye mkazi mwingine, Samwel Ndomba mkazi wa Njambe wilayani
humo alisema ni vigumu kwa sasa kupata samaki wanaoweza kutosheleza mahitaji ya
familia zao kwa bei ya chini, kwa sababu ya kupanda kwa bei hiyo ambayo
kwa watu wenye kipato cha kawaida wanashindwa kuimudu.
Ndomba alisema kuwa bei ya samaki imepanda kutoka shilingi 1,500
hadi shilingi 3,500 kulingana na ukubwa, huku hata dagaa ambao wanapatikana kwa
wingi katika ziwa Nyasa nao bei yake imepanda kutoka shilingi 4,000 hadi
shilingi 8,000 kwa dumla (sadolini).
No comments:
Post a Comment