Na Steven Augustino,
Tunduru.
MAWAZO Jabili (24) ambaye ni fundi maarufu wa kutengeneza
pikipiki aina ya Powertiller wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amefariki dunia
katika ajali mbaya ya pikipiki aliyokuwa akiiendesha.
Aidha katika ajali hiyo pia fundi msaidizi wa marehemu huyo,
aliyetambuliwa kwa jina la Abdalah Ngalibeyi naye amelazwa katika hospitali ya
wilaya hiyo, akiwa hajitambui baada ya kunusurika kifo katika ajali hiyo.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa, ajali hiyo
ilitokea kijiji cha Msinji kilichopo kata ya Ligoma wilayani humo.
Mjumbe wa Halmashauri ya kijiji hicho, Yassin Simonui alimwambia
mwandishi wetu kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 12.30 wakati watu
hao ambao walitokea Tunduru mjini, kwa ajili ya kwenda kutengeneza Powertiller katika
mashamba yaliyopo katika kijiji hicho.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi, aliokuwa
akiendesha pikipiki hiyo ambayo ni aina ya Sunlg yenye namba za usajiri T 445
AUD hali ambayo ilimfanya ashindwe kuimudu.
Mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Mawazo, Dkt.
Andreas Ndunguru alisema kuwa chanzo cha kifo hicho kilisababishwa na kutokwa
kwa damu nyingi baada ya kupata ajali hiyo.
Alisema katika ajali hiyo alipata majeraha kichwani na
kifuani, jambo ambalo lilisababisha kichwa chake kupasuka na kuufanya ubongo
kuchanganyika na damu.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji alithibitisha
kuwepo kwa ajali hiyo na kuongeza kwa kuwatahadharisha madereva wa vyombo vya
moto, kuwa makini pindi wanapoendesha vyombo hivyo ili kuokoa maisha yao na
abiria wanaowabeba.
Hata hivyo alisema endapo hawatakuwa makini katika udereva
wao, ipo hatari ya vijana wengi kuendelea kupoteza maisha na wengine kupata
ulemavu wa kudumu.
No comments:
Post a Comment