Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imesema kwamba,
itaendelea kufanya kazi ya kukamilisha ujenzi wa mfereji mkuu unaoleta maji shambani katika
skimu ya umwagiliaji Sangamabuni, iliyopo kijiji cha Mabuni kata ya
Litumbandyosi wilayani humo ili wakulima waweze kunufaika na kilimo cha zao la
mpunga kupitia umwagiliaji wanaoufanya katika mradi huo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Venance
Mwamengo alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambao
walitembelea kuona kazi ya kilimo cha zao la mpunga, kinachofanywa na kikundi
cha Sangamabuni kijijini humo.
“Hivi sasa tuna tatizo kubwa la ukosefu wa fedha katika
halmashauri yetu ili tuweze kukamilisha ujenzi wa miradi ya maendeleo ya
wananchi, lakini tunawaomba wananchi waendelee kuwa wavumilivu mara tupatapo
pesa tutaikamilisha ujenzi wake haraka iwezekanavyo”, alisema Mwamengo.
Mradi wa Sangamabuni ulianza kutekelezwa na wanakikundi
wenyewe mwaka 2011, ambapo hivi sasa wapo 122 wakiwemo wanawake 61 na wanaume
61 hivyo wanashindwa kufikia malengo ya uzalishaji kutokana na mfereji mkuu unaotumika
kupeleka maji shambani kutokamilika ujenzi wake.
Kwa mujibu wa Mwamengo alifafanua kuwa jitihada zilizooneshwa
na wakulima wa kikundi hicho, kuna kila sababu kwa serikali kuendelea kuunga
mkono ili waweze kuondokana na umaskini na kutumia fursa iliyopo kujiletea
maendeleo.
Hata hivyo aliwataka nao wataalamu wa ugani wilayani Mbinga,
kuendelea kuwa bega kwa bega na wakulima wanaozalisha mazao mbalimbali ya chakula
na biashara kwa kuwaelimisha mbinu bora za kilimo cha kisasa, ili waweze
kuzalisha mazao mengi yenye ubora na hatimaye kukuza uchumi wa wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment