Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WANANCHI wa kata ya Namtumbo wilaya ya Namtumbo mkoani
Ruvuma wamepongeza jitihada zinazofanywa na Kampuni ya Ilyana iliyopo mkoani humo, kwa kutoa msaada wa madawati kwa shule za msingi na sekondari ambazo zilikuwa zinakabiliwa na tatizo la upungufu madawati ya kukalia wanafunzi wanapokuwa darasani.
Khalfan Kigwenembe ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo inayofanya kazi ya kusafirisha abiria kutoka Songea kwenda Dar es Salaam,
alisema kuwa msaada wa madawati 220 yametolewa kwa shule hizo ambapo imekuwa ni
kawaida yao kutoa michango ya aina mbalimbali kwa wananchi wa kata hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini hapa,
Mkurugenzi huyo wa Ilyana alisema kuwa anayaomba makampuni mengine ambayo
yamewekeza katika mkoa huo waige mfano kama huo katika kuisaidia jamii, ili
iweze kuondokana na kero mbalimbali wanazokabiliana nazo.
“Wakurugenzi wengine wa makampuni mbalimbali nawaomba
watambue kwamba wanapowekeza wajue kuna kuisaidia jamii, ili waweze kunufaika
nayo kwa namna moja au nyingine kimaendeleo”, alisema Kigwenembe.
Alifafanua kuwa michango mingine aliyowahi kuitoa kipindi cha
nyuma katika kata ya Namtumbo kuwa ni madaftari 20,000 kwa kila shule za msingi
na sekondari, kwa ajili ya wanafunzi na ametoa ofa ya kusomesha watoto sita
kila mwaka wanaomaliza elimu ya msingi kwenda sekondari.
Vilevile aliongeza kuwa ametoa mchango wa shilingi milioni 2
kwa kuendeleza utengenezaji wa madawati na mifuko ya saruji, kwa ajili ya
kukarabati majengo ambayo ni chakavu kwa shule zote zilizopo katika kata hiyo.
No comments:
Post a Comment