Na Kassian
Nyandindi,
Njombe.
WANANCHI wa kata ya Mbalatse wilaya ya Makete mkoa wa Njombe,
wamemuomba Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvi kuona
umuhimu wa kuingilia kati mgogoro uliopo kati yao na mwekezaji wa Kampuni ya Silverlands Tanzania yenye makao yake makuu mkoani Iringa, ambaye anadaiwa kwamba amepora ardhi yao zaidi ya hekta 3,000
ambazo zilikuwa zikiwasaidia kuzalisha mazao ya aina mbalimbali.
Aidha kufuatia ardhi hiyo kuchukuliwa na mwekezaji huyo, wananchi
hao wanakosa maeneo ya kulima mazao ya chakula na biashara jambo ambalo hivi
sasa baadhi yao wanalazimika kwenda kwenye maeneo karibu na vyanzo vya maji
kulima mazao hayo.
William Lukuvi. |
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti,
wananchi hao walifafanua kuwa miaka iliyopita kwa muda mrefu walikuwa wakilima
mahindi kwa wingi katika eneo hilo ambalo ni maarufu kwa jina la Ludodolela,
ambalo lina rutuba tofauti na maeneo mengine yaliyopo kwenye kata hiyo.
Aloyce Chaula mkazi wa kijiji cha Mbalatse alifafanua kuwa
tangu kuzaliwa kwake miaka ya 60 iliyopita wazazi wake pamoja na wananchi
wengine wa kata hiyo walikuwa na mashamba yao katika eneo hilo ambalo amepewa
mwekezaji, bila wananchi kushirikishwa hivyo wanaiomba serikali kupitia Wizara hiyo
kunusuru hali hiyo ili wananchi wa kata hiyo waweze kurejeshewa mashamba yao.
“Ndugu waandishi wa habari mnaliona kundi hili kubwa la
wananchi wakilalamikia kuporwa maeneo yao, kwani awali huyu mwekezaji alikuja hapa
kwetu kijijini kuomba eneo dogo kwa muda kwa ajili ya kufanya majaribio ya
kupanda mbegu za zao la shairi, lakini tuna mshangaa ghafla amemilikishwa eneo
kubwa na sisi wazawa tumefukuzwa huku akiendelea na uzalishaji wa zao hili la
shairi”, alisema Chaula.
Kwa upande wake Damian Mwinuka mkazi wa kijiji hicho alieleza
kuwa kufuatia mwekezaji huyo kunyang’anya eneo hilo la mashamba bila kufuata
taratibu za utwaaji ardhi, hivi sasa vijana wengi wanakwenda mikoa ya jirani
kwenda kutafuta mashamba ya kulima wakati nyumbani kwao kulikuwa na eneo kubwa
la kuweza kuzalisha mazao mbalimbali ikiwemo viazi mviringo, ufuta, alizeti na
ngano.
Alisema kuwa kutokana na usumbufu huo wanaoupata sasa, bado
wanalazimika kuiangukia serikali ili iweze kuwasaidia na ardhi yao irejeshwe
mikononi mwao na sio vinginevyo.
Uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wa habari umebaini
pia katika mashamba hayo yanayolalamikiwa, mwekezaji huyo wa Silverlands Tanzania yenye makao makuu yake mkoani Iringa ndiyo
anayeendesha shughuli za kilimo cha zao la shairi kwenye eneo hilo
linalolalamikiwa na wananchi hao.
Waandishi hao wameshuhudia ndani ya eneo hilo kuna kiwanja
cha ndege ambapo inadaiwa kimekuwa kikitumika ndege kutua, kipindi cha kiangazi
wakati wa mavuno ya zao hilo na kwamba pia kumejengwa majengo ya ofisi na
nyumba za kuishi wafanyakazi wa shamba hilo.
Kadhalika sehemu ya shamba hilo kumezalishwa kwa wingi zao la
alizeti, ngano na mboga mboga pamoja na miti ya asili.
Naye diwani wa kata ya Mbalatse, Edson Msigwa alisema kuwa malalamiko
hayo ya wananchi ni ya kweli kwa kile alichodai kuwa mwekezaji huyo alipewa
ekari 70 tu kwa muda kwa lengo afanye majaribio ya kupanda mbegu za zao la
shairi, lakini anashangaa kuona amezalisha ekari zaidi ya 3,000 na
kujimilikisha maeneo hayo bila wananchi kujua.
Msigwa alisema kuwa kufuatia kuwepo kwa mkanganyiko huo, tayari
hatua zimechukuliwa kwa kwenda halmashauri ya wilaya ya Makete kuutaka uongozi
husika kuona namna ya kumaliza tatizo hilo, kabla machafuko hayajatokea kama
ilivyo kwa maeneo mengine ya nje ya mkoa wa Njombe.
“Wananchi wa kata yangu wapo tayari kufunga safari kwenda
kuonana na Waziri mwenye dhamana, ili waweze kupata haki zao za msingi juu ya
madai haya ya ardhi yao kutokana na hivi sasa wanakosa maeneo ya kuzalisha
chakula”, alisema Msigwa.
Pamoja na mambo mengine Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya
hiyo, Egnatio Mtawa alipohojiwa na waandishi wa habari alikiri kuwepo kwa
mgogoro huo na kuongeza kuwa tayari hatua zimeanza kuchukuliwa tume imeundwa
kuchunguza kwa undani juu ya jambo hilo, ambapo baadaye tume itatoa taarifa
baada ya kumaliza kazi yake.
Meneja wa shamba la kampuni hiyo,
Steven Maina alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya
malalamiko hayo ya wananchi, alikanusha na kusema kuwa hakuna mwananchi yeyote
aliyewahi kwenda ofisini kwake na kutoa malalamiko kama hayo huku akiongeza
kuwa kama kuna mtu anataka kufahamu juu ya umiliki wa shamba hilo, awasiliane
na uongozi wa kampuni hiyo na sio vinginevyo.
No comments:
Post a Comment