Na Kassian Nyandindi,
Njombe.
DIWANI wa kata ya Mbalatse wilayani Makete mkoa wa Njombe, Edson
Msigwa amesema kwamba amechukizwa na kitendo cha viongozi wa mkoa huo kufumbia
macho kwa muda mrefu malalamiko ya wananchi wake, juu ya kutwaliwa ardhi yao na
mwekezaji wa Kampuni ya Silverlands Tanzania yenye makao yake makuu mkoani Iringa bila kufuata taratibu husika, jambo ambalo linahatarisha kutokea kwa machafuko kati
ya wananchi na mwekezaji huyo.
Mkuu wa mkoa wa Njombe, Dkt. Rehema Nchimbi. |
Msigwa ambaye ni diwani wa kata hiyo, kupitia tiketi ya Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alisema kuwa licha ya kero hiyo kufikishwa
mezani kwa viongozi wa ngazi ya mkoa huo hakuna hatua zinazoonesha kuzaa
matunda hivyo kuna kila sababu kwa serikali, kuchukua hatua za haraka ili
kuweza kunusuru hali hiyo isiweze kuleta madhara hapo baadaye.
Hayo yalisemwa na diwani huyo alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari ambao walitembelea katika kata ya Mbalatse, kwa lengo la
kutaka kujua juu ya hatma ya mgogoro wa ardhi ambao umedumu kwa muda mrefu kati
ya wananchi na mwekezaji huyo.
Alisema kuwa tangu mwaka 1980 mwekezaji huyo aliingia katika
kata ya Mbalatse kwa ombi la kupewa ardhi ekari 70 ili aweze kufanya utafiti wa
kilimo cha zao la shairi, lakini anashangaa kuona kwamba amemilikishwa eneo la
zaidi ya hekta zaidi ya 3,000 bila kufuata taratibu za uchukuaji wa maeneo ya wananchi
wake kama sheria za nchi zinavyotaka.
“Wananchi wa Mbalatse wanajua kwamba ardhi yao inatumika kwa
manufaa ya watu binafsi sio kwa manufaa ya taifa, hivyo kupokwa kwa ardhi hii
zimetumika njia za hila na udanganyifu mkubwa”, alisema Msigwa.
Alifafanua kuwa hata uongozi wa kata hiyo haujui chochote
kinachoendelea katika mashamba hayo kufuatia ulinzi mkali ambao umewekwa na
mwekezaji, ambapo walinzi waliopo muda wote usiku na mchana wamekuwa na silaha
za moto ili kuzuia mtu yeyote asiweze kuingia katika eneo hilo.
Kadhalika Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete
Egnatio Mtawa alipohojiwa na waandishi wa habari, alikiri kuwepo kwa mgogoro
huo na kuongeza kuwa tayari hatua zimeanza kuchukuliwa tume imeundwa kuchunguza
kwa undani juu ya jambo hilo, ambapo baadaye itatoa taarifa baada ya kumaliza
kazi yake.
Naye Meneja wa shamba la kampuni ya Silverlands Tanzania,
Steven Maina wa eneo la Mbalatse alipoulizwa juu ya jambo hilo alikanusha na
kusema kuwa hakuna mwananchi yeyote aliyewahi kwenda ofisini kwake na kutoa
malalamiko hayo, huku akiongeza kuwa kama kuna mtu anataka kufahamu juu ya
umiliki wa shamba hilo awasiliane na uongozi wa kampuni hiyo na sio vinginevyo.
Hata hivyo Mkuu wa mkoa wa Njombe, Dkt. Rehema Nchimbi alipotakiwa
kutolea ufafanuzi juu ya hali hiyo aliwataka waandishi wa habari kwenda kumuona
Afisa mipango miji wa mkoa huo Sarah Seme, ambapo baada ya kuonana naye alikanusha
uwepo wa mgogoro huo wa ardhi katika kata ya Mbalatse na kuongeza kuwa wananchi
wa kata hiyo wanataka shamba hilo linaloendeshwa na mwekezaji huyo lirejeshwe mikononi
mwao, ili waweze kuzalisha mazao yao ya aina mbalimbali.
No comments:
Post a Comment