Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.
MKURUGENZI mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani
Ruvuma, Christopher Kilungu amewataka watendaji wa halmashauri hiyo kutekeleza
majukumu yao ya kazi, kwa kufuata misingi na taratibu zilizowekwa na serikali.
Aidha wakuu wa idara wametakiwa nao kuacha kuwa na majibu
mepesi ambayo hayajitoshelezi katika idara zao, pale watakapohitajika kutoa
ufafanuzi kuhusiana na kazi zao za kila siku.
Kilungu alisema hayo juzi alipokuwa kwenye kikao maalumu na
watendaji wa halmashauri ya Namtumbo kilichofanyika mjini hapa ambapo aliwataka
pia wakuu hao wa idara kufuata sera, kanuni, sheria na taratibu zilizowekwa
kwa kutumia taaluma zao.
Vilevile aliwataka kuwa wabunifu na
kushauri vitu vyenye manufaa kwa halmashauri hiyo na taifa
kwa ujumla, ili kuweza kuleta maendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na
baadaye.
Pia aliwataka wakuu hao wa
idara kumpa ushirikiano wa dhati katika kusimamia maendeleo
ya wananchi, huku akiongeza kuwa yeye amepewa dhamana na
serikali katika kuhakikisha kwamba halmashauri ya Namtumbo inasonga mbele
kimaendeleo.
“Ndugu zangu tuchape kazi kwa uhakika, tuache majungu na
fitina nawataka tufanye kazi kwa vitendo sio maneno”, alisisitiza Kilungu.
No comments:
Post a Comment