Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
UJENZI wa stendi kuu ya magari ya abiria Manispaa ya Songea
mkoani Ruvuma, umeingia dosari kufuatia Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania
(JWT) tawi la Songea mkoani humo, kuinyoshea kidole Halmashauri ya Manispaa
hiyo kutokana na kujenga uzio kwenye eneo hilo ambalo wanatambua kuwa ni sehemu
ya makazi ya watu wakifanyia biashara zao za aina mbalimbali.
Aidha walisema kuwa wameshangazwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa
Manispaa hiyo kupuuza ombi la kumtaka asitishe ujenzi wa uzio huo wa tofari zilizotengenezwa
kwa a saruji mpaka atakapokaa na wafanyabiashara hao, ili waweze kuona namna
gani ujenzi unafanyika ili kuweza kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida Julai Mosi mwaka huu majira
ya mchana, baadhi ya wanajumuiya ya wafanyabiashara hao Songea mjini
walikusanyika na kwenda katika eneo hilo la stendi kuu, kupinga ujenzi huo
usifanyike mpaka kero zao zitakaposikilizwa na viongozi wa halmashauri hiyo.
Tukio hilo ambalo lilishuhudiwa na waandishi wa habari, Nico
Challe ambaye ni Katibu wa wafanyabiashara hao alisema wameamua kufanya hivyo
baada ya kuona viongozi wa Manispaa hiyo, wamekuwa wakijichukulia maamuzi peke
yao bila kushirikisha wadau husika.
“Malalamiko na mombi ya wafanyabiashara katika kituo hiki cha
mabasi yaliandikwa kwa barua tangu Mei 30 mwaka huu, kwenda kwa Mkurugenzi wa
halmashauri hii tukimtaka asitishe ujenzi mpaka tutakapokaa pamoja na
kushauriana namna ya kufanya, lakini cha kushangaza tumepuuzwa hakuna majibu
yoyote tuliyopewa na ujenzi kama hivi unaendelea”, alisema Challe.
Naye January Ndumbaro ambaye naye pia ni mfanyabiashara katika
eneo hilo, alifafanua kuwa ujenzi huo umesababisha kuharibu hata miundombinu ya
maji ya bomba na kusababisha bomba hilo linalopeleka maji kwa wakazi wa mtaa wa
Mfanyaranyaki mjini hapa, kukosa huduma kutokana na miundombinu husika
kuharibiwa.
Aliongeza kuwa hata vibanda vyao ambavyo wamevijenga ndani ya
eneo hilo la biashara wameambiwa wavibomoe kwa madai kwamba wanapaswa kupisha,
ili katika eneo hilo lililopo na vibanda hivyo liweze kujengwa kibanda cha
kupumzikia abiria huku mkataba wake, akiwa kama mpangaji ukionesha muda wake
bado haujaisha.
Kadhalika mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Sabina
Mkalanga aliongeza kuwa kuna kila sababu kwa mamlaka husika, kuona umuhimu wa namna
ya kumaliza kero hiyo iliyojitokeza na sio kulazimisha kwa matakwa yao binafsi
bila kushirikisha jamii.
Ujenzi wa uzio huo katika eneo la stendi kuu ya mabasi ya
abiria Songea mjini, unafanywa na mkandarasi ambaye amewekwa na Halmashauri
hiyo ambapo hata kibao kinachoelekeza ujenzi huo hakijawekwa na kwamba wakati
wafanyabiashara hao wanaingia katika eneo la stendi hiyo kupinga ujenzi wa uzio
usiendelee kufanyika, mtu mmoja ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake akidaiwa
kuwa ndiye msimamizi mkuu anayesimamia ujenzi huo alikimbia na kutokomea
kusikojulikana baada ya kuona kundi hilo la watu likielekea katika eneo la
ujenzi unapofanyika.
Alipoulizwa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya
Songea, Jenifer Homoro alithibitisha kuwepo kwa malalamiko hayo na kuwataka
waandishi wa habari kwenda kumuona Mhandisi wa ujenzi wa Manispaa hiyo, Godfery
Majuto ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya kero hiyo.
Hata hivyo Majuto alipohojiwa alisema kuwa uzio huo unajengwa
baada ya Madiwani wa halmashauri hiyo, kuketi kupitia vikao husika na
kukubaliana ujenzi ufanyike ili kuweza kuzuia watu kuingia hovyo na halmashauri
kukusanya mapato yake kwa ufanisi mzuri.
No comments:
Post a Comment