Na Kassian Nyandindi,
Songea.
KAIMU Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na Usafi wa
Mazingira Manispaa ya Songea (SOUWASA) mkoani Ruvuma, Mhandisi John Kapinga
amesikitishwa na idara ya ujenzi katika Manispaa hiyo kuharibu miundombinu ya
bomba la maji katika eneo la Stendi kuu ya mabasi ya abiria, ambalo hupeleka
huduma hiyo muhimu kwa wakazi wa mtaa wa Mfaranyaki mjini hapa.
Leonidas Gama, Mbunge wa Songea mjini. |
Uharibifu huo umefanyika kufuatia msingi uliochimbwa katika
eneo la bomba kuu la kupeleka maji katika mtaa huo kwa lengo la kujenga uzio,
katika eneo hilo la stendi ili watu wasiweze kuingia hovyo na Manispaa kuweza
kukusanya mapato yake.
Masikitiko hayo ya Mkurugenzi huyo wa SOUWASA yalitolewa
mbele ya waandishi wa habari, ambao walikwenda Ofisini kwake kwa lengo la
kutaka kujua kwa nini ukuta huo unaojengwa katika eneo hilo la stendi ujengwe juu
ya bomba hilo ambalo endapo litaharibika wakati wowote ule, Mamlaka hiyo baadaye
itakapohitaji kulifanyia marekebisho itashindwa kutokana na kujengwa kwa uzio
huo kwa kutumia tofari za saruji.
Kapinga alisema taratibu za ujenzi huo hawajashirikishwa na
kwamba haiwezekani bomba hilo la maji lijengwe kwa ajili ya kuhudumia jamii
halafu juu yake, ujengwe ukuta huo bila wao kujua na kutoa ushauri namna ya
kutekeleza jambo hilo.
“Manispaa yetu kuna mapungufu makubwa ya ushirikishwaji, jambo
hili mnalotuambia ndio kwanza tunalisikia kutoka kwenu ninachojua haya yote
yanatokana na ushirikishwaji kutoka kwa hawa wenzetu viongozi wa Manispaa hii kuwa
mdogo, lakini wangeweza kutushirikisha tungewapatia ushauri mzuri nini
wakifanye”, alisema Kapinga.
Akifafanua juu ya wananchi kulalamikia kuharibiwa kwa bomba
hilo alisema kuwa watafuatilia suala hilo, kuweza kuona ni namna gani
linatengenezwa haraka ili kuweza kurejesha huduma husika kwa wananchi na kuweza
kuondokana na adha wanayoipata sasa ya kukosekana kwa huduma ya maji.
Kaimu Mkurugenzi huyo wa Mamlaka ya maji safi na Usafi wa
Mazingira katika Manispaa ya Songea, aliongeza kuwa anashangazwa na ujenzi wa
uzio huo katika eneo hilo la stendi kuu kwani unawafanya kuharibu mipango yao
ya ujenzi wa tenki kubwa la maji hapo baadaye, ambalo inabidi lijengwe kwa
ajili ya kuendelea kupanua mtandao wa huduma ya maji safi kwa wananchi.
“Katika eneo hilo pia tunatarajia kujenga tenki kubwa la maji
sasa leo hii wanapojenga uzio huu tutapita wapi, vitu kama hivi walipotaka
kuvifanya walipaswa kutushirikisha”, alisema.
Pamoja na mambo mengine alipoulizwa Mhandisi wa ujenzi wa
Manispaa ya Songea, Godfrey Majuto alisema kuwa changamoto za mabomba ya maji
huwa wanakutana nazo mara nyingi pale wanapotaka kufanya shughuli za ujenzi wa
miundombinu husika katika Manispaa hiyo.
Majuto alieleza kuwa anaushangaa uongozi wa Mamlaka hiyo ya
maji safi na Usafi wa Mazingira katika Manispaa ya Songea, kusema kwamba jambo
hilo hawakushirikishwa wakati taratibu za ujenzi wa uzio wa stendi hiyo zinafanyika.
No comments:
Post a Comment