Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Ruvuma, imewataka
wananchi wake kudai risiti wanaponunua bidhaa dukani huku ikiwasisitiza wafanyabiashara
wenye maduka hayo, kuhakikisha kwamba wanatoa risiti za Kieletroniki (EFD’S)
kwa wateja wao bila kuwepo usumbufu wa aina yoyote ile.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi ofisini kwake, Meneja wa TRA mkoani
humo Rosalia Mwenda alisema kuwa Mamlaka hiyo imetoa matangazo yake yenye kusisitiza
kuwa mwananchi atakayeshindwa kudai risiti kwa mfanyabiashara husika wakati wa
kununua bidhaa na mfanyabiashara huyo, akabainika kushindwa kutoa risiti ni
makosa kufanya hivyo na kwamba wote kwa pamoja wakikamatwa watashtakiwa na
serikali.
Mwenda alifafanua kuwa sheria inamtaka anayeuza bidhaa ya
aina yoyote ile dukani anatakiwa kutoa risiti na mnunuzi pia kudai risiti,
kinyume na hapo wasipofanya hivyo wanakuwa wametenda kosa.
Alibainisha kuwa mnunuzi anapodai risiti asipopewa na muuzaji,
anatakiwa kwenda kumshtaki ofisi za Mamlaka ya Mapato popote pale zilipo ili
sheria iweze kuchukua mkondo wake, lakini pia naye mnunuzi huyo asipodai na
akabainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua na sio vinginevyo.
Alieleza kuwa kazi kubwa ya TRA ni kukusanya, kukadiria na
kuhasibu mapato ya serikali, hivyo ili kodi ikadiriwe kwa viwango vya uhakika
ni vyema uwepo umuhimu wa wafanyabiashara, kujenga tabia ya kuwa karibu na mamlaka
hiyo ili wasipate usumbufu wa kulipa kodi kulingana na biashara zao wanazofanya.
Kadhalika Meneja huyo wa Mamlaka ya mapato mkoani Ruvuma,
Mwenda aliwaomba wafanyabiashara wa wilaya zote za mkoa huo kuona umuhimu wa
kulipa kodi kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza baadaye na
kwamba ikibainika baadhi yao wamekuwa wakikwepa kulipa kodi, hatua kali za
kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Nawaomba wafanyabiashara wetu ni vyema wafike ofisi za TRA
kwa ajili ya kukadiriwa mahesabu ya biashara zao, ili waweze kulipa kodi ya
serikali kwa wakati na waache tabia ya kukwepa kulipa kodi”, alisisitiza Mwenda.
No comments:
Post a Comment