Ofisi za makao makuu ya Kampuni ya Tutunze Kahawa Limited (TKL) zilizopo Mbinga mjini. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WADAU wa maendeleo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma
wameipongeza Kampuni ya Tutunze Kahawa Limited (TKL) iliyopo wilayani hapa, kwa
jitihada zake za kuunga mkono na kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ya
wananchi wilayani humo.
Pongezi hizo zilitolewa juzi mjini hapa, wakati kampuni hiyo
ilipokuwa ikikabidhi madawati 20 yenye thamani ya shilingi milioni 1.9 kwa
uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kukalia wanafunzi shuleni.
Walisema kuwa juhudi hizo zinazofanywa na TKL kuna kila
sababu kwa makampuni mengine yaliyopo wilayani Mbinga, kuiga mfano huo katika
kuchangia michango ya maendeleo ili wilaya hiyo iweze kusonga mbele na kukua
kiuchumi.
Aidha naye Meneja masoko wa kampuni hiyo, Thomas Ngapomba kwa
upande wake alisema kuwa katika juhudi za kuunga mkono kampeni iliyoanzishwa na
Rais Dkt. John Magufuli ya kuondoa tatizo la madawati kwa shule za msingi na
sekondari hapa nchini, Tutunze Kahawa Limited nayo iliona kuna umuhimu wa kuchukua
jukumu la kuchangia madawati hayo kwa wilaya ya Nyasa na Mbinga.
Ngapomba alifafanua kuwa lengo la kufanya hivyo ni
kuhakikisha kwamba wanafunzi wanakuwa na mazingira mazuri ya kusomea, pale
wanapokuwa darasani ili waweze kuandika mwandiko mzuri.
Alisema kuwa tokea kampuni hiyo ianzishwe mwaka 2009 wilayani
humo na kujishughulisha na biashara ya zao la kahawa, imeweza kutoa michango yenye
thamani ya shilling milioni 34.9 katika sekta ya elimu, afya na jamii kwa
ujumla.
Vilevile alibainisha kuwa shule ya Makita sekondari iliyopo Mbinga
mjini ilikabidhiwa msaada wa kompyuta tano na vifaa vya kufundishia tekinolojia
ya mawasiliano, huku shule ya Lusetu sekondari iliyopo katika kata ya Luwaita,
jengo la shule hiyo lenye vyumba viwili vya maabara vilifanyiwa ukarabati.
“Mifuko 250 ya saruji, ukarabati wa maabara kwenye shule za
sekondari wilayani Mbinga tumekuwa tukiufanya na pia shule ya sekondari Kikolo
iliyopo kata ya Kikolo wilayani hapa, tumetoa mchango wa mifuko 40 ya saruji
kwa ajili ya kukarabati vyumba vya madarasa”, alisema Ngapomba.
Kadhalika alisema kuwa Maguu sekondari iliyopo kata ya Maguu,
Dkt. Shein sekondari kata ya Mpepai walipewa mchango wa mifuko 50 ya saruji kwa
kila shule, Mikiga sekondari Mbinga mjini ilipewa mabati 100 na mifuko 30 ya
saruji kwa ajili ya kukamilisha ukarabati vyumba vya madarasa na kwamba
wamekarabati pia mfumo wa kuleta maji safi, kwenye kijiji cha Myangayanga kwa
kukarabati mabomba na viunganishi vyake.
“Tumeshiriki pia kikamilifu katika kuboresha mazingira kwa
kufanya usafi katika mji wa Mbinga, tumefunga vifaa vya nguvu ya sola kwenye
zahanati ya kijiji cha Nyoni kata ya Nyoni”, alisema.
Kwa wilaya ya Nyasa katika kipindi cha mwaka huu,
kampuni hiyo ya Tutunze Kahawa Limited imechangia kwa kutoa vifaa vya kufanyia
ukarabati nyumba ya mganga zahanati ya kijiji cha Kingirikiti kata ya
Kingirikiti wilayani humo, vyenye thamani ya shilingi milioni 8,000,000 pamoja
na mchango wa madawati 20 ya kukalia wanafunzi darasani yenye thamani ya
shilingi milioni 1.9.
No comments:
Post a Comment