Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA kuhakikisha kwamba agizo la serikali la kuboresha
ukusanyaji wa mapato yake linatekelezwa ipasavyo, halmashauri ya wilaya ya
Mbinga mkoani Ruvuma imejiwekea mikakati ya kununua na kusambaza mashine za Kieletroniki
(EFD’S) katika vijiji vyote vilivyopo wilayani humo.
Aidha hadi kufikia mwezi Julai mwaka huu, imeweza kununua
mashine hizo 20 zenye thamani ya shilingi milioni 17 na kuanza kuzisambaza
katika maeneo husika ambako tayari zimeanza kufanya kazi iliyolengwa.
Taarifa hiyo ilitolewa na Mweka hazina wa halmashauri ya
wilaya Mbinga, Joseph Mazito alipokuwa akiwasilisha mada husika kwa Madiwani wa
halmashauri hiyo katika mafunzo elekezi ya ukusanyaji mapato ndani ya wilaya
hiyo.
Mazito alifafanua kuwa mpango wa halmashauri yake ni kupeleka
mashine hizo katika vijiji vyote 118 vilivyopo wilayani humo na kwamba mpaka
sasa watendaji husika, wanaofanya kazi ya kukusanya mapato wamekwisha pewa
mafunzo juu ya namna ya kutumia mashine hizo.
“Waheshimiwa Madiwani, tunaomba mtambue kwamba mtu ambaye
atakuwa mbali na suala hili la ukusanyaji mapato mjue kwamba huyo hatufai
katika kufikia lengo la maendeleo ya wilaya yetu, tumchukulie hatua”,
alisisitiza Mazito.
Aliongeza kuwa mategemeo ya halmashauri ya Mbinga, hadi
kufikia mwezi Desemba mwaka huu watakuwa wamepeleka mashine zote za kukusanyia
mapato kwenye kila kijiji, huku akiwataka Madiwani hao kujenga ushirikiano na
wataalamu wake ndani ya wilaya ili kuweza kufikia malengo hayo waliyojiwekea.
Mweka hazina huyo alisisitiza kwamba, kwa mtu yeyote
atakayebainika anakwepa kulipa ushuru atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo
kufikishwa Mahakamani na kutozwa faini kulingana na kosa alilofanya, hivyo
amewataka watendaji husika waliopewa dhamana ya kusimamia suala hilo kuwa
makini katika utendaji wa kazi zao.
Kufuatia uwepo wa mikakati hiyo kwa upande wao, Madiwani hao
walisema hawatakubali kuona uzembe unafanyika katika utekelezaji wa zoezi hilo
hivyo wapotayari kuhakikisha kwamba, wanakuwa bega kwa bega ili mapato yao yaweze
kukusanywa kikamilifu na kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi
katika maeneo husika wilayani humo.
No comments:
Post a Comment