Na Muhidin Amri,
Songea.
CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT) mkoani Ruvuma, kimepongeza
juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya wamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt.
John Magufuli kwa kukusanya kodi, kupambana na vitendo vya wizi, ufisadi na
uzembe mahali pa kazi.
Aidha chama hicho kinaamini kwamba, hatua hiyo itasaidia
kupatikana kwa fedha ambazo zitalipa madeni mbalimbali wanayoidai walimu
serikali, ambapo kipindi cha nyuma ulipaji wake ulikuwa ukisuasua na kuwavunja
moyo watumishi hao waliopo katika sekta ya elimu.
Hayo yalisemwa jana na Katibu wa CWT mkoani hapa, Shaibu
Mohamed alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake mjini Songea.
Mohamed alisema kuwa licha ya serikali kuanza kuchukua hatua
dhidi ya watumishi wasiofaa ambao kwa muda mrefu wameliingizia taifa hili
hasara kubwa, bado kuna umuhimu wa kuendelea na msako huo hata kwa watumishi wa
ngazi ya juu ambao baadhi yao wanatumia vyeti na majina bandia kujipatia
ajira katika idara na taasisi za umma.
Pia Katibu huyo ameishauri serikali kushughulikia tatizo la
vyeti bandia hata kwa wanafunzi wa vyuo mbalimbali hapa nchini,
ikiwemo vyuo vya ualimu kwa kuwa tatizo hilo limeshamiri kwa wanafunzi wa vyuo
vingi vya ualimu hapa nchini.
Alifafanua kuwa katika kushughulikia tatizo hilo, wamiliki wa
vyuo watungiwe sheria itakayowabana wamiliki husika kupeleka kwanza vyeti vya
wanafunzi hao wanaojiunga katika baraza la mitihani la taifa, ili wachunguzwe
kama wanavyeti halali au la.
“Serikali ikifanya hivyo itasaidia wanafunzi wanaoingia na wale
wanaomaliza kwenye vyuo hivyo kuwa na sifa ya kushika nafasi mbalimbali za
uongozi, wataweza kuwa waadilifu na wachapakazi ambao watakuwa tayari
kuwatumikia Watanzania wenzao”, alisema Mohamed.
Aliongeza kuwa CWT inasikitishwa na kuzagaa kwa veti bandia
pamoja na vitendo vya watumishi hewa ambao wengi wao, hawana sifa ya kuongoza
au kufanya kazi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Kadhalika alieleza kuwa hata mpango wa kutoa elimu bure
kuanzia shule za msingi hadi sekondari utafanikiwa tu, endapo serikali
itamaliza kulipa madeni ya walimu, kitendo ambacho kitasaidia kurudisha moyo wa
utendaji kazi zao za kila siku.
Alibainisha kwamba hadi kufikia mwezi Julai mwaka huu, walimu
wa shule za msingi mkoani Ruvuma wanaidai serikali kiasi cha
shilingi milioni 403.3 za mishahara, huku walimu wa sekondari nao wakidai shilingi
milioni 114 mbali na madeni mengine kama vile uhamisho na kupanda kwa madaraja.
No comments:
Post a Comment