Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEBAINISHWA kuwa, endapo halmashauri ya wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma itapima ardhi yake katika vijiji na miji midogo iliyopo wilayani humo, itaweza
kukusanya kodi ya shilingi bilioni 6.7 kila mwaka kupitia ardhi husika
iliyopimwa.
Kodi hiyo itakayokusanywa itatokana na heka 67,000 ambazo
wataalamu wa ardhi wataanza kufanya kazi ya kupima wilayani humo, mapema kuanzia
mwezi huu na kukamilisha kazi hiyo katika kipindi cha miezi mitatu.
Hayo yalibainishwa na Mthamini wa ardhi halmashauri ya wilaya
ya Mbinga Gabriel Kameka, alipokuwa akiwaelimisha Madiwani wa wilaya hiyo kwenye
mafunzo elekezi ya siku moja yaliyolenga juu ya ukusanyaji mapato kwa
halmashauri hiyo.
“Hili suala ni lazima tulivalie njuga sisi sote, tujenge
ushirikiano tuweze kufanikiwa kama hatutakuwa pamoja ni sawa na kutwanga maji
kwenye kinu”, alisema Kameka.
Kameka alisema kuwa Madiwani wanapaswa huko waendako
wakawaelimishe wananchi wao, ili zoezi hilo litakapoanza kutekelezwa pasiwe na
vikwazo vya aina yoyote ile.
Alisema kuwa, ikumbukwe kwamba ardhi iliyopimwa mwananchi
ananufaika nayo kwa njia mbalimbali, ikiwemo kwanza ni dhamana kwake kufuatia
hati aliyonayo inamfanya aweze kukopa kwenye taasisi za kifedha na kumwezesha
kufanya shughuli zake za maendeleo.
Ili halmashauri iweze kupata mapato yake kupitia ardhi,
alisema ni lazima ipimwe na wamiliki husika wawekeze kwenye ardhi hiyo ndipo
mapato hupatikana zaidi.
Kwa upande wao Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga
walisema kuwa wanafurahishwa na mipango hiyo ya kimaendeleo inayotekelezwa na
wataalamu wake, hivyo waliahidi huko waendako kwenda kusimamia kikamilifu jukumu
hilo walilopewa kwa kutoa elimu kwa wananchi wao ili nao waweze kushiriki
kikamilifu.
No comments:
Post a Comment