Askari akiwa amewakamata viongozi wawili wa serikali ya
Kijiji waliokuwa wakituhumiwa kuhujumu viwanja vya wananchi.
|
Na Kassian Nyandindi,
Tunduru.
MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Juma Homera amewatia
mbaroni viongozi wanne wa serikali ya vijiji kwa kosa la usimamizi mbovu wa
ardhi katika vitongoji vya Umoja na Frank Weston vilivyopo katika kata ya
Nanjoka wilayani humo.
Akisoma taarifa mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo, Yahaya Abdallah
alimweleza Mkuu wa wilaya Homera kuwa vitongoji hivyo vimekumbwa na mgogoro wa
ardhi kwa muda mrefu kati ya wenyeji, wageni na wafanyakazi wa halmashauri ya wilaya
Tunduru.
Abdallah alisema kuwa serikali kupitia idara ya ardhi na maliasili
wilayani humo iliwapimia ardhi wananchi wake tokea mwezi Agosti 2014 lakini
ikabainika kwamba mpaka kufikia mwezo Juni mwaka huu, bado wananchi wa
maeneo hayo hawakupewa ardhi yao huku orodha ikionesha kuwa baadhi ya
wafanyakazi wa halmashauri pamoja na wageni wapo kwenye orodha ya wananchi
wanaopaswa kugawiwa viwanja hivyo.
Akihutubia kwenye mkutano huo wa hadhara uliyofanyika katika
shule ya msingi Umoja, Homera aliwaeleza wananchi kuwa wasiwe na shaka kwa
sababu serikali ipo upande wao na hakuna atakaye dhulumiwa haki yake.
Ilibainika kuwa kuna baadhi ya watumishi wa idara ya ardhi na
maliasili wilayani humo, ambao wamefanya ujanja ujanja kinyume cha sheria kwa
kuwaweka watoto wao kwenye orodha ya majina ya wale wanaotakiwa kupewa viwanja.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Homera alisema hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi yao ili kuweza kuondoa mgongano uliopo ambao unatishia
usalama wa wananchi hao.
Pia ilielezwa kuwa kumekuwa na baadhi ya viongozi wanatuhumiwa
kukusanya fedha za wananchi wapatao 522 na kutowapatia risiti, jambo
ambalo imeleezwa kuwa ni hujuma za wazi za kuikosesha halmashauri ya wilaya
hiyo mapato yake.
Kufuatia hali hiyo aliwataka wafanyakazi wa idara ya ardhi na
maliasili wilayani humo, kujieleza ni kwa nini wamegawa viwanja kwa watu ambao
sio wahusika jambo ambalo linadhihirisha wazi kuwa ni udanganyifu mkubwa ambao
haupaswi kufumbiwa macho.
Kwa upande wake Mkuu wa idara ya ardhi na maliasili wilayani
Tunduru, Japhet Mnyagala alikiri kufanya makosa hayo na kumhakikishia Mkuu wa wilaya
hiyo, ndani ya wiki moja wananchi wataanza kugawiwa viwanja vyao na kero hiyo
itakuwa imekwisha.
Hali ilibadilika baada ya muda mfupi ambapo Mkuu wa wilaya,
Homera aliwaagiza askari wake wakamate viongozi waliokuwa wasimamizi wa upimaji
wa maeneo hayo katika vitongoji vya Umoja na Frank Weston ambao ni Mohamed
Dumsala, Matola Limelime, Halid Daud na Tekla Damas.
No comments:
Post a Comment