Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
MKUU wa Polisi wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Shaban Mpwaga amemshukuru
na kumpongeza Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa
wilaya hiyo, Cassian Njowoka kwa kutoa msaada wa tairi nne za gari la kituo kikuu
cha Polisi wilayani humo zenye thamani ya shilingi milioni 4.4.
Aidha alisema kuwa gari la kituo hicho ambalo tairi zake
zimekuwa kipara, wakati mwingine askari wake wanashindwa kutekeleza majukumu
yao kikazi kutokana na tairi zilizopo kwisha muda wake wa matumizi.
Shukrani hizo zilitolewa jana na Mkuu huyo wa Polisi wilaya
ya Nyasa kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya msaada huo, iliyofanyika katika
viwanja vya kata ya Kingirikiti wilayani hapa.
Mpwaga alifafanua kuwa licha ya kupewa msaada huo pia Njowoka
siku za nyuma aliwahi kuwapatia msaada wa kompyuta, printa mbili za kisasa na
karatasi rimu katoni mbili kwa ajili ya kuweza kusaidia kufanyia kazi za Polisi
kama vile kuchapa barua za aina mbalimbali.
Kwa upande wake Kamanda wa UVCCM wilayani humo, Njowoka
alisema kuwa kutokana na mahusiano ya chama na serikali kuwa mazuri hivyo
aliona kuna kila sababu kutoa msaada huo, ili uweze kusaidia jamii katika
kutekeleza majukumu ya kimaendeleo.
Njowoka alieleza kuwa hata wananchi wengine ambao ni wazawa
wa wilaya hiyo ambao wanaishi nje ya Nyasa, wanapaswa kuwa na moyo wa kwenda
kusaidia wananchi kwa kutoa michango ya kimaendeleo ili wilaya iweze kupiga
hatua mbele za maendeleo kwa haraka.
“Sisi tuliozaliwa katika wilaya hii na waalika wananyasa wenzangu
wote popote pale walipo, wakumbuke kuja kuwekeza na kutoa michango
itakayotufanya tupige hatua mbele na kukuza uchumi wetu”, alisema.
No comments:
Post a Comment