Sunday, August 28, 2016

MKURUGENZI MADABA AFUNGA CHUO FEKI CHA UUGUZI

Na Kassian Nyandindi,      
Songea.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma Shafii Mpenda amelazimika kukifunga chuo cha Noble College Tanzania Limited (NCTL) ambacho kilikuwa kinatoa mafunzo ya uuguzi baada ya kubaini kwamba chuo hicho, hakijasajiliwa kisheria na miundo mbinu yake sio rafiki kwa wanafunzi wanaosomea taaluma hiyo.

Shafii Mpenda.
Mpenda alisema kuwa amefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa katika halmashauri yake hakuna mtu yeyote ambaye amewahi kupeleka maombi kwa ajili ya uendeshaji wa mafunzo ya uuguzi, jambo ambalo limesababisha kuwepo kwa malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi kwamba chuo hakina usajili unaotambuliwa na serikali.

Alifafanua kuwa kuanzia sasa NCTL hakitaruhusiwa kutoa mafunzo ya uuguzi na amewataka wanafunzi wamtafute mkuu wa chuo hicho, ili aweze kuwarejesha majumbani kwao kwani kuna baadhi ya wanafunzi wanatoka mikoa ya Kigoma, Shinyanga, Iringa, Njombe, Rukwa na Tabora hapa nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa chuo hicho Kelvin Sikamanga, alipohojiwa na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na kufungwa kwa chuo chake alithibitisha kuwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Mpenda amekifunga chuo chake kwa madai kwamba hakina sifa na hakijasajiliwa, lakini amefafanua kuwa chuo hicho alikwisha kisajili chini ya mwamvuli wa chama cha msalaba mwekundu.


Alisema kuwa tangu alipokisajili chuo hicho, Septemba 28 mwaka 2015 kimepokea wanafunzi wa kozi ya mwaka mmoja ambao wanachukua mafunzo ya huduma ya kwanza na sio uuguzi kama inavyoelezwa.

Baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika chuo cha NCTL wameuomba uongozi wa chuo kuangalia uwezekano wa kuwarudishia fedha walizolipia karo, ili waweze kurejea makwao na kwamba Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, Zubery Kitimbe alieleza kwamba wamekuwa wakipatiwa mafunzo mazuri ya uuguzi na huduma ya kwanza.

Mganga mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Damas Kayera alipoulizwa kuhusiana na chuo hicho kufungwa alikiri kuwa katika orodha ya vyuo vya kitabibu katika mkoa wa Ruvuma, chuo hicho hakipo na kwamba amewataka wazazi wa wanafunzi wanaosoma hapo wafanye utaratibu mwingine wa kuwahamisha wanafunzi kwenda vyuo vingine vinavyotambulika kisheria.


Kayera alisema kuwa chuo hicho hakijasajiliwa kisheria kutoa huduma ya kwanza pamoja na ya uuguzi hivyo, hakina walimu wenye sifa za kufundisha taaluma hiyo na kwamba majengo yake hayana hadhi pia ya kutolea huduma husika.

No comments: