Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKUU wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Palolet Mgema ameonya
vikali dhidi ya kikundi cha baadhi ya Madiwani wa Manispaa ya Songea mkoani
humo ambao walitaka kuleta fujo wakati wa kikao cha baraza la madiwani
kilichoketi juzi mjini hapa, ambapo amesema kwamba endapo kama watarudia tena
atawachukulia hatua za kisheria.
Aidha Mgema alisema kuwa kamwe hataweza kuvumilia kuanzia
sasa kuona tabia hiyo inajirudia tena na kwamba, akijitokeza mtu yeyote na
kusababisha kuleta vurugu zinazoashiria uvunjifu wa amani atakiona cha
mtemakuni.
Mgema alisema hayo kwenye kikao cha baraza la madiwani
kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa mjini Songea, kufuatia kutokea kwa mvutano
mkali kati ya baadhi ya kikundi cha madiwani wachache wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
na Meya wa halmashauri hiyo, Abdul Mshaweji kuhusiana na hoja ya mabasi ya
kupakia abiria kuanzia stendi kuu ya zamani iliyopo mjini hapa kwenda Msamala
iliyopo mbali na mji huo.
Hali hiyo ilizua tafrani ndani ya kikao hicho na kuwafanya
baadhi ya wananchi waliohudhuria kuwazomea madiwani ambao walikuwa wakipindisha
hoja hiyo kwa nguvu na kuwaunga mkono, Meya Mshaweji pamoja na Mbunge wa Songea
mjini Leonidas Gama ambao walionyesha wazi kuwasaidia wananchi kutatua kero hiyo
ya muda mrefu ya ombi lao la mabasi kuanzia stendi hiyo ya zamani.
Wakati wa kujadili hoja hiyo kikundi cha baadhi ya madiwani
wachache walionekana kutoridhishwa na maamuzi ya madiwani wengi, ambao
waliwatetea wananchi kwa kukubali mabasi ya abiria yaanzie katika stendi hiyo
ili kuweza kuwaondolea wananchi adha waliyokuwa wakiipata kwa muda mrefu ya
kwenda kupanda mabasi eneo la Msamala ambalo lipo mbali na mji wa Songea.
Mkuu huyo wa wilaya alifafanua kuwa kama diwani anahoja yake
muhimu binafsi anapaswa kufuata taratibu husika, kwa kuwasilisha hoja hiyo
katika mfumo ulio rasmi na sio kukurupuka ndani ya kikao na kutaka kusababisha
vurugu zisizokuwa na msingi wa aina yoyote ile.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Songea, Mshaweji baada
ya kuona madiwani hao hawamsikilizi huku baadhi yao wakisimama ndani ya kikao
na kuchangia hoja bila kufuata taratibu, aliwaonya na kumuomba Mkuu wa wilaya
hiyo, Mgema kuingilia kati kutoa karipio la kutaka kuwatoa nje ya ukumbi ndipo
baadaye waliweza kutulia.
Akichangia hoja wakati wa kikao hicho naye diwani wa kata ya
Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Rashid
Mososa alisema yeye haoni dhambi mabasi hayo kupakia na kushusha abiria katika
stendi hiyo ya zamani.
No comments:
Post a Comment