Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa kitendo cha askari Polisi wa wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma wengi wao kuishi uraiani, kwa kiasi kikubwa kunachangia
kutotimiza majukumu yao ya kazi ipasavyo, hivyo serikali imeombwa kuona
uwezekano wa kutatua kero hiyo.
Aidha nyumba zilizopo ambazo baadhi yao wanaishi, zimekuwa
chakavu ambapo nyakati za masika huwa zinavuja na hilo linatokana na bati
zilizoezekwa kuwa na matundu yanayopitisha maji ya mvua.
Hayo yalisemwa leo na askari hao walipokuwa wakizungumza na
Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Sixtus Mapunda, ambaye aliwatembelea kwa ajili
ya kuzungumza nao na kusikiliza kero zao mbalimbali.
Walisema kuwa hata jengo la ofisi za kituo kikuu cha Polisi
wilaya ya Mbinga hali yake ni mbaya, ambapo linahitaji kufanyiwa ukarabati ili
liweze kuwa kati hali nzuri.
Ramia Mganga ambaye ni Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo, alisema
hayo wakati alipokuwa akitoa taarifa fupi kwa Mbunge huyo ambapo alieleza kwamba
kuna tatizo sugu la nyumba za kuishi askari wake, ambapo zaidi ya asilimia 80
wamekuwa wakipanga uraiani.
Mganga alifafanua kuwa askari hao wamekuwa wakifanya kazi
katika mazingira magumu na kwamba, wanahitaji kupewa pikipiki bora za kisasa
kwa ajili ya kuimarisha zoezi la ulinzi shirikishi katika kata mbalimbali wilayani
Mbinga.
Kwa upande wake Mbunge, Mapunda mara baada ya kusikiliza
matatizo hayo alitoa ahadi ya kukarabati jengo la kituo hicho cha Polisi kwa
kulipaka rangi pamoja na nyumba moja wanayoishi askari wageni ambao huwasili
kufanya kazi wilayani humo, atalifanyia ukarabati kwa kuezua bati chakavu
zilizopo sasa na kuezeka bati mpya ili lisiendelee kuleta madhara kwa watumiaji
hasa nyakati za masika.
“Tunathamini mchango wenu mkubwa mnaoutoa katika nchi hii,
tuendelee kushirikiana kwa kuiweka Mbinga yetu wakati wote katika hali ya
usalama ili wananchi waweze kufanya maendeleo yao na kukuza uchumi wetu”,
alisema Mapunda.
Pamoja na mambo mengine Mbunge huyo alisema kuwa kero hizo zilizopo
kwa askari wake wa wilaya ya Mbinga, atazifikisha kwa Waziri mwenye dhamana ili
ziweze kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu ikiwemo hasa juu ya suala la ujenzi wa
nyumba za kuishi askari hao.
No comments:
Post a Comment