Waziri wa nishati na madini, Profesa Sospeter Muhongo. |
Na Mwandishi wetu,
Kagera.
BAADHI ya Wateja ambao wamelipia huduma ya kuunganishiwa nishati
ya umeme majumbani kwao wilaya ya Biharamulo mkoa wa Kagera, wamelinyoshea
kidole Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) wilayani humo kwa kushindwa
kutimiza majukumu yake kwa wakati na kuwafanya wateja hao, wapate hasara katika
kuendesha shughuli zao za ujasiriamali.
Aidha imeelezwa kuwa wateja hao ambao ni wa maeneo ya mjini wamelilalamikia
Shirika hilo wakidai kwamba, tokea walipolipia huduma ya kujengewa mita za
umeme mwanzoni mwa mwezi wa sita mwaka huu, hakuna utekelezaji uliofanyika
jambo ambalo linawafanya wawe na mashaka.
Wakizungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, walisema
kuwa shughuli zao za ujasiriamali ambazo zinategemea nishati hiyo ya umeme
wanashindwa kuziendesha, hivyo wanaiomba serikali itatue kero hiyo mapema ili
waweze kuondokana na adha kubwa wanayoipata sasa.
Kadhalika wamemuomba Waziri mwenye dhamana, Profesa Sospeter
Muhongo kuona umuhimu wa kuingilia kati ili kuweza kumaliza tatizo hilo mapema ambalo
hawajui litakwisha lini.
Lazaro Daud ambaye ni mkazi wa Biharamulo mjini, akizungumza
kwa niaba ya wateja wenzake alieleza kuwa kila anapokwenda kufuatilia suala
hilo makao makuu ya ofisi za TANESCO wilayani humo, hakuna majibu sahihi
anayopewa na kwamba wapo zaidi ya wateja 80 ambao wamekuwa wakilalamikia hali
hiyo kwa muda mrefu.
“Hata shughuli zetu za ufundi seremala zimesimama tunashindwa
kuendesha viwanda vyetu vidogo vidogo kutokana na tatizo hili, hivi sasa
tumekata tamaa kwani tumelipia kwa muda mrefu hakuna huduma tuliyopata”,
alisema Daud.
Kwa upande wake alipohojiwa kwa njia ya simu Meneja wa
shirika hilo wilayani Biharamulo, Ernest Milyango alikiri kuwepo kwa tatizo
hilo huku akieleza kuwa limetokana na kukosekana kwa vifaa husika vitakavyoweza
kukamilisha kazi ya kuwaunganishia umeme wateja hao majumbani kwao.
Milyango aliongeza kuwa mfumo wa manunuzi unaofanyika makao
makuu ya Ofisi za TANESCO Dar es Salaam baada ya wao kupeleka orodha ya vifaa
husika nao huchangia kuchelewa kuwaletea vifaa hivyo, kwani huchukua muda mrefu
na kuwafanya wateja wao walalamikie hali hiyo kutokana na kukosa huduma husika.
“Nafikiri hawa wateja wetu watuvumilie kidogo, tatizo kubwa
hapa ni suala la vifaa, baadhi yake vimekwisha letwa tunasubiri mpaka
vikamilike ndipo wakati wowote kuanzia sasa tutaanza kazi ya kuwajengea mita za
umeme”, alisema Milyango.
No comments:
Post a Comment