Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
MTOTO Zawadi Hassan (14) mkazi wa kitongoji cha Majengo
kijiji cha Mkongo wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, amejinyonga kwa kutumia
chandarua chake wakati akiwa chumbani kwake baada ya kuchoshwa na kauli
zisizokuwa na staha kutoka kwa mama yake mzazi ambaye hakufahamika
jina lake mara moja.
Tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki ambapo
mwili wa marehemu huyo ulikutwa chumbani kwake asubuhi siku ya Ijumaa, baada ya
mama huyo kumtaka aamke na ndipo jitihada za kumwita mlangoni ziligonga mwamba
ambapo alipochukua jukumu la kufungua mlango, aliukuta mwili wa mwanae ukiwa
juu unaning’inia.
Mtendaji wa kata ya Mkongo, Whiclif Mtinda alikwenda katika
eneo la tukio na kuthibitisha kifo cha kijana huyo kilichosababishwa na kujinyonga
kwa kutumia chandarua kutokana na kauli za kuudhi kutoka kwa mama
yake mzazi.
Kwa mujibu wa Mtinda alieleza kuwa kabla ya kwenda
kulala marehemu alikuwa anadai hela yake kutoka kwa mama yake ambazo
alimpatia mama huyo amwekee na alipozihitaji, mama huyo alikuwa akimtolea
maneno yasiyokuwa mazuri na ndipo mtoto huyo aliamua kuchukua maamuzi hayo
magumu.
Malumbano ya mama na mwanae yaliendelea na kumtaka mwanae
aondoke na aende kuishi na baba yake mzazi, kwa kuwa baba ya mtoto huyo na
mama yake waliachana miaka mingi iliyopita.
“Kitendo cha mama huyu kumweleza mtoto wake aende akaishi
kwa baba yake na kumnyima fedha zake alizoziweka kwake, ndipo alikasirika
na kuamua kujinyonga”, alisema Mtinda.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji
amethibitisha kujinyonga kwa mtoto huyo ambapo marehemu amezikwa katika kijiji
cha Mkongo na kwamba Polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.
No comments:
Post a Comment