Mji wa Songea. |
Na Muhidin Amri,
Songea.
WATU waliopo katika makundi maalum katika Manispaa ya Songea
mkoani Ruvuma, wamepatiwa mafunzo ya kuzuia maambukizi mapya ya Virusi vya
ugonjwa wa Ukimwi ili waweze kuepukana na maambukizi hayo.
Zaidi ya watu 80 ndio waliopewa mafunzo hayo ya siku mbili
mjini hapa, ambapo makundi hayo yalipata elimu juu ya ukweli kuhusu Virusi Vya
Ukimwi (VVU) na UKIMWI, matumizi sahihi ya kondomu ikiwemo za kike na kiume
pamoja na madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya.
Mratibu wa Ukimwi na tiba Manispaa ya Songea, Dkt. Felista Kibena
alisema makundi ambayo yamenufaika na mafunzo hayo ni watu wanaofanya biashara
ya ngono, wanaofanya ngono ya jinsia moja na watu wanaojidunga sindano
pamoja na watumiaji wa unga na madawa hayo ya kulevya.
Kibena alisema kuwa idara yake imeamua kutoa elimu hiyo juu
ya ukweli kuhusu magonjwa hayo, baada ya utafiti kubaini kwamba makundi hayo
sasa yanaongoza kwa kiwango kikubwa cha maambukizi.
Alifafanua kuwa njia ambazo zinaongoza kwa maambukizi mapya
ya ukimwi ni kupitia ngono ya kawaida isiyo salama na mtu aliyehatarini
au aliyeambukizwa kutoka kwa mama aliyeambukizwa kwenda kwa mtoto wakati wa
kujifungua au kunyonyesha.
Njia nyingine ni Kupitia sindano
zilizoambukizwa kwa watumiaji wa dawa za kulevya kwa njia ya
sindano, kupitia njia ya ulawiti kwa mwanamume kwa mwanamume kwa mwanamume kwa mwanamke
na kupitia uchangiaji wa vifaa vya kuchanjia au kudungia na wakati
wa tohara.
“Tumefanikiwa kutoa elimu ya kutosha kuzuia maambukizi ya
virusi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, hali hiyo imesababisha watoto
waliozaliwa na VVU wamekuwa na afya nzuri baada ya kuwaanzishia dawa za
kurefusha maisha (ARVS) na hivi sasa wengi wao wanasoma sekondari na vyuo
vikuu’’, alisema.
Mratibu huyo aliongeza kuwa utafiti umebaini kwamba matumizi
ya dawa za kulevya hasa kwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 45 bado
ni tatizo kubwa katika Manispaa ya Songea mkoani hapa.
Kwa upande wake, Ofisa habari wa Manispaa hiyo Albano Midello
alisema kuwa takwimu zilizopo mjini hapa zinaonesha kuwa katika kipindi cha
mwaka 2015 kulikuwa na waathirika wa dawa za kulevya 145 kati ya hao wanaume
138 na wanawake walikuwa saba.
Alieleza kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi
Mei mwaka huu Manispaa hiyo ina jumla ya waathirika wa dawa hizo 97 kati yao,
wanawake wawili na wanaume 95 ambapo waathirika wote hawa wakiwa na umri
kati ya miaka 15 hadi 45.
No comments:
Post a Comment