Na Muhidin Amri,
Songea.
MBUNGE wa Songea mjini mkoani Ruvuma Leonidas Gama amewaeleza
wakuu wa idara halmashauri ya Manispaa Songea kwamba, nchi ya Tanzania hivi
sasa imebadilika na mabadiliko hayo ni ya kudumu, endelevu na wala sio nguvu ya
soda hivyo wanapaswa kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea badala yake
wanapaswa kuwatumikia wananchi ipasavyo.
Leonidas Gama. |
Gama alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na wakuu hao wa
idara akiwa ameambatana na Meya wa Manispaa hiyo Abdul Mshaweji, katika kikao kilicholenga kupanga
mikakati itakayosaidia kujenga ubunifu wa kuboresha vyanzo vya mapato na kukuza
uchumi wa manispaa hiyo kwa manufaa ya jamii.
“Tanzania ni nchi ambayo imebadilika na mabadiliko haya ni ya
kudumu, sio nguvu ya soda, Rais Dkt. John Magufuli hapendezwi na mambo yaende
hovyo hovyo, hivyo watumishi mnapaswa kuacha kufanya kazi kwa mazoea”, alisema.
Pia alisisitiza kwa kuwataka wataalamu hao kuangalia namna ya
kuondoa kero za wananchi ikiwemo ukarabati wa barabara kwenye mitaa na kata,
kero ya maji safi na salama, kushughulikia migogoro ya ardhi na kuzuia vitendo
vya ujenzi holela.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo, amewaagiza watendaji hao
kukusanya mapato kwa utaratibu uliowekwa na serikali kwa kutumia mfumo wa
mashine za Kieletroniki (EFD’S), ambao hudhibiti mapato ya serikali na
hatimaye kuweza kusaidia kuboresha huduma za wananchi.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Songea, Abdul Mshaweji
amewapongeza watumishi hao kwa kazi ya kusimamia maendeleo ya wananchi, lakini
aliwataka kuhakikisha mpango kazi mpya unaoanza mwaka huu wa fedha kuhakikisha
malengo yake yanatekelezwa ipasavyo.
“Ninyi wakuu wa idara ndiyo nguzo muhimu ya maendeleo ya
wananchi, hivyo nawataka msichanganye utaalamu mlionao na mambo ya kisiasa, ili
tuweze kutoka hapa tulipo tunahitaji kuchapa kazi kwa kujituma”, alisisitiza
Mshaweji.
Ameagiza kuzingatia na kuheshimu sheria ndogondogo zilizowekwa
ndani ya Manispaa hiyo, ikiwemo kujenga ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato na kuwa
na nidhamu nzuri ya matumizi ya fedha za serikali.
No comments:
Post a Comment