Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia Injinia Stella
Manyanya amesema kwamba serikali hapa nchini, itaendelea kushirikiana na
madhehebu yote ya dini katika kuhakikisha kwamba amani na utulivu ni jambo ambalo,
linapaswa kuwepo wakati wote kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Aidha ameitaka jamii kuona umuhimu wa kupeleka watoto wao
shule, ili waweze kusonga mbele kimaendeleo na kulifanya taifa liweze
kuondokana na tabaka la watu maskini.
Injinia Stella Manyanya. |
Vilevile alisisitiza kwamba, serikali haitasita kuwachukulia
hatua wazazi ambao wataonekana wanakwamisha jitihada za maendeleo ya mtoto
shuleni ikiwemo kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria kama vile mahakamani.
Injinia Manyanya alisema hayo leo alipokuwa mgeni rasmi,
wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya Jubilei ya kutimiza miaka 25 ya Upadri
jimbo la Mbinga, yaliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Killian lililopo
mjini hapa.
Maadhimisho hayo yalihusisha mapadri 11 wa kutoka Parokia
mbalimbali zilizopo jimboni humo, tangu walipopata upadirisho wao Septemba 13
mwaka 1991 katika utumishi wao wa kuwatumikia wakristo wenzao.
Mapadri hao ni Philibert Mbunda, Alfredy Komba, Aidan
Nchimbi, Mendrad Nyandindi, Thadei Kinyero, Christopher Mapunda, Amon Nchimbi,
Addo Mapunda, Thimoth Ndunguru, Joackimu Lipanga na Bosco Ndiu.
“Ndugu zangu wakristo, tuendelee kumuomba Mungu katika
shughuli zetu za kimaendeleo, bila kufanya hivi mambo yote
tunayoyafanya hapa duniani ni sawa na bure, hatuwezi kufikia malengo yetu
tuliyojiwekea pasipo kutekeleza hili”, alisisitiza Manyanya.
Awali akitoa hati za baraka kwa mapadri hao, zilizotolewa na
Baba Mtakatifu Papa Francis wa Kanisa katoliki duniani mbele ya waumini
waliohudhuria misa takatifu ya maadhimisho hayo, Askofu mstaafu wa Jimbo la Mbinga
Dkt. Emmanuel Mapunda aliwataka mapadri hao waliotimiza miaka 25 ya utumishi
wao wa kikristo kuacha kumpiga vita Askofu aliyekuwa madarakani, John Ndimbo.
Pia Dkt. Mapunda alisisitiza kwa kuwataka wampatie
ushirikiano wa kutosha katika kutimiza majukumu yake ya msingi, ili kuweza
kuendelea kudumisha ukristo katika jimbo hilo.
Hata hivyo Askofu huyo aliongeza kuwa mapadri hao,
wanapaswa kumuomba Mungu kwa mapungufu yao waliyoyafanya au yaliyojitokeza
wakati wa ukuhani wao wa kulitumikia kanisa katika kueneza dini ya kikristo ili
waweze kuwa na maisha marefu.
No comments:
Post a Comment