Na Kassian Nyandindi,
Songea.
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Ruvuma
kimesema kwamba kinapinga vikali katazo la vikao vya ndani vya chama,
lililotolewa na Jeshi la Polisi hapa nchini kupitia kwa Mkuu wa Oparesheni na
mafunzo ya jeshi hilo, CP Nsato Marijani.
Akizungumza na mwandishi wetu jana ofisini kwake Mwenyekiti
wa CHADEMA mkoani hapa, Ireneus Ngwatura
alisema kuwa tayari maandalizi yao ya Oparesheni UKUTA mkoani hapa yamekamilika
kwa asilimia 99.
“Kuhusu katazo hili la vikao vya ndani ambalo limetolewa na
Jeshi la Polisi kwamba kuanzia Agosti 24 mwaka huu ni marufuku kufanya vikao
vya ndani vya kisiasa kwa vyama vya siasa, jambo hili kwetu halikubaliki kabisa
na wala hakuna mwanachama yeyote atakayeridhia katazo hili”, alisema Ngwatura.
Ngwatura alieleza kuwa viongozi wa mkoa wa Ruvuma wa CHADEMA
wameona kuna umuhimu wa kuwahimiza wanachama wake wa wilaya zote, kwamba
ifikapo Septemba Mosi mwaka huu kutakuwa na maandamano kama yalivyopangwa na si
vinginevyo.
Alisema kuwa kabla ya siku hiyo ya maandamano, wanatarajia
kufanya mikutano ya ndani katika kila wilaya zilizopo mkoani humo ambapo wataanzia
ngazi ya kijiji, kata, wilaya na mkoa.
Vilevile Ngwatura alisema jambo la pili ambalo anapenda
kulifikisha kwa Watanzania wote ni kuhusu Oparesheni UKUTA inayotarajiwa
kufanyika Septemba 1 mwaka huu, ambayo ni moja kati ya maazimio ya kikao cha
Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Taifa, kilichofanyika Julai 23
hadi 26 mwaka huu maandamano ya mikutano ni lazima yafanyike na kwamba ni haki
ya mwananchi kikatiba na kisheria kufanya hivyo.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, alipohojiwa
kuhusiana na sakata hilo la maandamano hayo alisema kuwa Jeshi la Polisi mkoani
humo lilikwishawapelekea CHADEMA mkoa wa Ruvuma zuio la kuwataka wasifanye
mikutano ya ndani na maandamano yoyote yale ya kichama, ambayo wanatarajia
kuyafanya na badala yake amewahimiza kuona umuhimu wa kwenda kufanya kazi ili
kuwaletea maendeleo wananchi wakiwemo wanachama wao.
Kamanda Mwombeji alisisitiza kuwa mwanasiasa yeyote
atakayekaidi zuio hilo atashughulikiwa kisheria na kwamba kwa mtu yeyote mwenye
uelewa anapaswa aheshimu katazo hilo na sio vinginevyo.
No comments:
Post a Comment