Na Mwandishi wetu,
Songea.
BAADHI ya wananchi wa kijiji cha Lyangweni kata ya Litapwasi
wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wamekumbwa na hali mbaya baada ya kuhofiwa
kunywa kinywaji aina ya togwa kinachodaiwa kuwa na sumu.
Wananchi hao ambao ni 66 walikunywa kinywaji hicho wakati
walipokuwa kwenye sherehe ya mwananchi mwenzao, ambaye jina lake halikuweza
kufahamika mara moja.
Habari zilizopatikana mjini hapa ambazo zimethibitishwa na
Mganga mkuu wa wilaya hiyo Dkt. Yesaya Mwasubira, alisema kuwa tukio hilo
lilitokea juzi majira ya mchana huko katika kijiji cha Lyangweni ambacho kipo
umbali wa kilometa tisa kutoka Songea mjini.
Alisema kuwa wanakijiji hao walikuwa wamekwenda kwenye sherehe
hiyo, ambako walipatiwa chakula pamoja na kinywaji aina ya togwa
iliyotengenezwa kienyeji.
Kadhalika baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wetu
kwa nyakati tofauti walisema kuwa togwa hiyo, ilikuwa imeandaliwa kwa wingi
kwenye sherehe hiyo na kila aliyekunywa baada ya muda mfupi tu, alianza kulalamika
kuuma tumbo.
Walisema kuwa baadaye wote waliokuwa wamekunywa, hali zao
zilizidi kuwa mbaya ndipo uongozi wa kijiji ulilazimika kuchukua hatua kwa
kutoa taarifa kwenye Ofisi ya mtendaji wa kata, ambaye ndiye aliyechukua hatua
ya kuwasiliana na uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Songea juu ya tukio hilo.
Walifafanua kuwa baada ya masaa matatu kupita, timu ya
wataalamu wa afya iliwasili kijijini hapo na kuanza kutoa huduma ya kwanza kwa
waathirika wote ambao walifikishwa kwenye zahanati ya kijiji cha Lyangweni, walipatiwa
matibabu na kuruhusiwa kurudi majumbani kwao licha ya kwamba hali zao zilikuwa
bado sio nzuri.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Songea ambaye pia ni diwani
wa kata ya Litapwasi Rajabu Mtiura alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusiana na tukio
hilo, alisema tayari waathirika wote waliokunywa togwa hiyo wametibiwa na
wanaendelea kupata matibabu katika zahanati hiyo.
“Tukio hilo ni la pili kutokea hapa kwetu, la kwanza
lilitokea mwaka mmoja uliopita katika kijiji cha Litapwasi wanakijiji zaidi ya
200 waliokuwa kwenye sherehe ya Kipaimara, waliugua matumbo yao na kulazwa
kwenye kambi maalumu baada ya kunywa togwa iliyodaiwa kuwa inasumu”, alisema
Mtiura.
Vilevile Mganga mkuu wa wilaya hiyo, Dkt. Mwasubira
alifafanua kuwa wagonjwa waliofika kwenye Zahanati hiyo wamepewa dawa za
kutosha na hali zao zinaendelea vizuri na kwamba timu ya wataalamu wa afya, bado
wapo kwenye kijiji hicho wakisubiri kuangalia afya za waathirika hao.
“Tayari hatua zimechukuliwa kwa kuchukua sampuli na masalia
ya kinywaji hiki walichokunywa aina ya togwa, kwa ajili ya kupeleka kwa mkemia
mkuu wa serikali ili tuweze kubaini chanzo cha tukio hili”, alisema.
Jitihada ya kumpata Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma,
Zubery Mwombeji ziligonga mwamba baada ya simu yake ya kiganjani kuita kwa muda
mrefu bila kupokelewa.
No comments:
Post a Comment