Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WATENDAJI wa vijiji na kata katika Halmashauri ya wilaya ya
Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kukusanya mapato ya halmashauri hiyo kwa
kuhakikisha kwamba wanadhibiti mianya inayoweza kupoteza mapato hayo, ili fedha
zitakazopatikana ziweze kwenda kufanya kazi za maendeleo ya wananchi.
Vilevile wameagizwa kuendelea kuimarisha mfumo wa ukusanyaji
mapato hayo kwa kutumia mfumo wa mashine maalumu za kieletroniki (EFD’S) ili
kuweza kudhibiti wizi unaoweza kutokea kwa wale watendaji wasiokuwa waaminifu
ambao wamekuwa na mazoea ya kuiibia serikali.
Gombo Samandito ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri
ya wilaya ya Mbinga, alisema hayo juzi alipokuwa akitoa maelekezo mbalimbali ya
kikazi kwa watendaji hao katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika
mjini hapa.
“Tujitahidi kuziba mianya inayoweza kupoteza mapato ya
halmashauri yetu, watendaji wote tunapaswa mtusaidie kusimamia ukusanyaji wa
mapato tuimarishe mifumo yetu ya ukusanyaji, ili tuweze kufikia ipasavyo
malengo yetu tuliyojiwekea”, alisema Samandito.
Pia alitoa agizo kwa kuwataka wataalamu husika wa halmashauri
ya wilaya ya Mbinga, kuanza mara moja zoezi la upimaji wa maeneo ya wazi ili
kuweza kutenga maeneo ya makazi, uwekezaji wa viwanda vikubwa na vidogo.
“Ni vyema ndugu zangu wakati wa upimaji tusisahau kutenga
maeneo haya kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi wetu, pia kwa faida ya kizazi
cha sasa na baadaye”, alisema.
Alisisitiza kwamba jukumu kubwa la viongozi wa serikali ni
kuwahudumia wananchi ipasavyo, hivyo kiongozi yeyote katika eneo lake
akishindwa kutekeleza majukumu yake aliyopewa maana yake ameshindwa kuwajibika
na kwamba yupo tayari kumchukulia hatua kali za kisheria, ikiwemo kumfukuza
kazi.
No comments:
Post a Comment