Na Mwandishi wetu,
Namtumbo.
KUFUATIA kutolewa
kwa orodha ya majina ya wadaiwa sugu ya mkopo wa elimu ya juu,
kumeibuka taharuki kwa baadhi ya watumishi wa wilaya ya Namtumbo mkoani
Ruvuma kuingizwa kwenye orodha ya wadaiwa hao, licha ya kutosoma elimu ya
juu na kutohusika kuomba mkopo huo.
Kwa mujibu
wa Ofisa habari wa wilaya hiyo, Yeremias Ngerangera amethibitisha kupokea
malalamiko kutoka kwa walimu sita wa shule za msingi wilayani humo ambao
wanadai kuwa hawajasoma elimu hiyo ya juu na hawakuomba fedha hizo kutoka bodi
ya mikopo.
Aidha Ngerangera aliwataja
walimu waliowasilisha malalamiko yao wilayani humo kuwa ni mwalimu Thomas Komba
ambaye anadaiwa shilingi 3,444,030, Joseph Chengura anayedaiwa 12,911,370 na mwalimu Michael Haulle anayedaiwa shilingi 2,733,099 na
bodi ya mikopo elimu ya juu.
Vilevile
aliwataja wengine kuwa ni mwalimu Michael Jimmy anayedaiwa shilingi
29,125,905 mwalimu Deogratias Haulle anayedaiwa shilingi 16,055,100
na Marry Haulle anayedaiwa shilingi 2,643,518 ambao wote wanailalamikia
bodi hiyo kwa kuingizwa kwenye orodha ya madeni hayo wakati wao
hawajawahi kuomba fedha hizo kwa ajili ya kwenda kusoma.
Ofisa habari huyo
wa wilaya ya Namtumbo alifafanua kuwa halmashauri ya wilaya hiyo
inaendelea kupokea malalamiko kama hayo ya walimu wote wa shule
za msingi na sekondari kwa maandishi, ili yaweze kuwasilishwa kwenye bodi ya mikopo kwa uchunguzi na kuchukuliwa hatua zaidi.
Walimu hao
walikwenda kwa Ofisa habari huyo kuelezea masikitiko yao juu ya kuingizwa kwenye orodha ya madeni ya wadaiwa sugu, huku wakidai kuwa
endapo serikali haitaweza kuchukua hatua dhidi ya wahusika waliofanya ujanja
huo wapo tayari kuomba msaada wa kisheria popote pale ili waweze kumaliza
tatizo hilo.
Hata hivyo uongozi husika wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, umewataka
walimu wote kuwasilisha vielelezo vyao mapema wakiwemo na watumishi wengine ambao
wanadai kwamba hawakusoma elimu ya juu huku wakati huo wakiwa wameingizwa
kwenye orodha ya wadaiwa sugu, ili kuweza kupeleka malalamiko yao kwa bodi ya
mikopo kwa uchunguzi wa madai yao.
No comments:
Post a Comment