Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linamshikilia Filbert Moyo
(40) mkazi wa kijiji cha Tingi wilaya ya Nyasa mkoani humo kwa kukutwa na silaha
mbili aina ya Gobole ambazo zimetengenezwa kienyeji.
Aidha Jeshi hilo linamsaka mtu mwingine ambaye jina lake halikuweza
kufahamika mara moja, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Malumba wilayani Tunduru mkoani
hapa kwa kukutwa na silaha aina ya SMG ikiwa na risasi 23.
Zubery Mwombeji, Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma. |
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake, Kaimu
kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Dismas Kisusi alisema kuwa tukio la kwanza
lilitokea Agosti 13 mwaka huu majira ya saa 11:30 asubuhi huko katika wilaya ya
Nyasa ambako askari Polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa na
silaha hizo.
Kisusi alisema kuwa silaha hizo alikuwa amezihifadhi kwenye
mfuko katika eneo la Ngurumashamba kwenye hifadhi ya wanyama ya Liparamba iliyopo
wilayani humo.
Alifafanua kuwa Polisi walipata taarifa kwamba Moyo anamiliki
silaha kinyume na sheria za nchi ndipo walipokwenda huko kumfuatilia, walifanikiwa
kumkamata na kwamba upelelezi juu ya tukio hilo bado unaendelea kufanywa utakapokamilika
atafikishwa Mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.
Kadhalika alilitaja tukio jingine kuwa Agosti 14 mwaka huu
majira ya asubuhi huko katika kitongoji cha Malando kijiji cha Malumba tarafa
ya Nalasi wilayani Tunduru askari Polisi wakiwa kwenye doria,
walifanikiwa kumkamata mtu mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara
moja na baadaye aliwakimbia na kuitupa silaha moja aina ya SMG yenye namba za
usajili 1952 KMI.
Alieleza kuwa katika silaha hiyo kulikuwa na risasi 23 na
kwamba tukio hilo lilitokea karibu na ofisi ya kijiji hicho na jitihada ya
kumsaka mtuhumiwa huyo zinaendelea.
Hata hivyo Kisusi alitoa rai kwa mtu yeyote anayetumia au
kumiliki silaha kinyume na taratibu za nchi ni vyema akaona umuhimu wa kusalimisha
silaha yake mara moja, ili zifanyiwe uchunguzi na wamiliki halali wazisajiri
mapema kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment