Basi hilo lenye namba za usajili T 830 CWZ likiwa limeteketea moto.(Picha na Kassian Nyandindi) |
Songea.
ABIRIA 28 waliokuwa wakisafiri kwa basi la Kampuni ya Sajda
kutoka Mbinga mjini kwenda Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamenusurika kupoteza
maisha yao kufuatia basi hilo walilokuwa wakisafiria kuteketea kwa moto.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery
Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 1 mwaka huu majira ya jioni saa
11:45 katika eneo la Minazi, kijiji cha Kigonsera wilayani Mbinga.
Mwombeji alifafanua kuwa tukio hilo lilihusisha basi lenye
namba za usajili T 830 CWZ aina ya Mitsubishi Rosa, ambalo ni mali ya Hamis
Said mkazi wa Songea mjini mkoani hapa.
Alibainisha kuwa gari lilikuwa likiendeshwa na Rashid Mohamed
(38) anayeishi Songea mjini ambapo chanzo cha tukio hilo, kilitokana na injini
ya gari kuanza kuwaka moto ghafla wakati likiwa katika mwendo kasi barabarani.
“Baada ya dereva kuona gari linatoa moshi kutoka kwenye
injini alisimama ghafla na abiria wote waliokuwemo kwenye gari haraka
waliteremka wakiwa salama na mizigo yao, hakuna aliyepoteza maisha lakini basi lote
limeteketea kabisa”, alisema Mwombeji.
Hata hivyo Kamanda huyo wa Polisi hapa mkoani Ruvuma, ametoa
wito kwa wamiliki wa magari yanayosafirisha abiria mkoani humo kuyafanyia
matengenezo kikamilifu magari yao mara kwa mara, kabla hayajaanza safari
barabarani ili kuweza kuepukana na majanga yanayoweza kutokea na kupoteza nguvu
kazi ya taifa hili.
No comments:
Post a Comment