Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linawasaka watu wanaodaiwa
kuhusika kuwashushia kipigo kikali kwa kuwapiga kwa mapanga, mawe na marungu watu
wawili sehemu mbalimbali za miili yao ambao ni wakazi wa kijiji cha Ndumbi na
Lituhi, wilaya ya Nyasa mkoani humo na kuwasababishia vifo papo hapo.
Zubery Mwombeji. |
Mauaji hayo yalitokana na watu hao wakituhumiwa kwamba
ni washirikina ambapo walimpoteza kimazingara, kijana mmoja aliyefahamika kwa
jina la Baraka Mahundi (28) katika ziwa Nyasa.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba amewataja waliouawa kuwa ni
Jackob Mahundi (90) mkazi wa kijiji cha Ndumbi na Vicent Ngatunga (63) wa kijiji
cha Lituhi wilayani humo.
Alifafanua kuwa tukio hilo limetokea Agosti 24 mwaka huu
majira ya usiku katika kijiji cha Ndumbi kata ya Mbaha wilayani humo, ambapo
inadaiwa siku hiyo ya tukio watu wote wawili hao walipigwa wakiwa huko pamoja na
kupoteza maisha yao.
Mwombeji alieleza kuwa chanzo cha tukio hilo kinatokana
na madai ya kutuhumiwa kuhusika na vitendo vya ushirikina vilivyosababisha kumpoteza
kijana Baraka Mahundi, ambaye alikwenda katika ziwa Nyasa kuvua samaki Agosti
16 mwaka huu na kwamba mpaka sasa kijana huyo hajapatikana.
Alisema kuwa juhudi za kukisaka kikundi cha watuhumiwa
walioshiriki katika tukio hilo la mauaji, zinaendelea kufanywa ili watuhumiwa
waweze kupatikana na kufikishwa kwenye vyombo vya dola kujibu tuhuma
inayowakabili mbele yao.
No comments:
Post a Comment