Na Julius Konala,
Songea.
WAANDAAJI wa shindano la kumsaka mrembo wa Miss Ruvuma mwaka
huu, kutoka Rona Promotion ya Jijini Dar es salaam kupitia ufadhili wa Kampuni
ya Bayauck ya nchini Japan, wametoa msaada wa nguo mbalimbali kwa baadhi ya
wazee wasiojiweza katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma zenye thamani ya
zaidi ya shilingi milioni 1,000,000.
Msaada huo ulitolewa juzi kwa wazee hao na washiriki wa
shindano hilo kupitia shirika la kuhudumia wazee (PADI) lililopo mjini hapa ambapo
Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Rona promotion Nassib Mahinya, alisema kuwa
wameamua kufanya hivyo baada ya kuguswa na changamoto mbalimbali zinazowakabili
wazee.
Mahinya alisema kuwa lengo kuu ni kuwafundisha washiriki wa
mashindano ya warembo, kujitoa katika kusaidia jamii na makundi mengine yasiyojiweza
huku akifafanua kuwa mapato yatakayopatikana siku ya shindano hilo
litakalofanyika Agosti 27 mwaka huu, asilimia 10 itaelekezwa kusaidia jamii.
Naye mmoja wa washiriki wa shindano hilo Irene Msabaha, alisema
amezitaka taasisi, mashirika na watu binafsi wenye mapenzi mema kuunga mkono
juhudi hizo za kuwasaidia wazee kwa madai kuwa, bado wanakabiliwa na changamoto
nyingi katika maisha yao.
Kwa upande wake mwakilishi toka shirika la kuhudumia wazee (PADI)
Ndaisaba Jackson aliwashukuru waandaaji wa shindano hilo, kwa kuona umuhimu wa
kuwasaidia wazee hao huku akidai kuwa kundi hilo bado linakabiliwa na
changamoto ya afya, chakula, mavazi na malazi.
Pamoja na mambo mengine, washindi watatu wa mwanzo
watakaopatikana katika shindano hilo watashiriki kwenye shindano la Kanda ya
nyanda za juu kusini ambalo linatarajiwa kufanyika Septemba 9 mwaka huu kwa
kushindana na warembo toka mikoa ya Iringa, Mbeya, Rukwa, Katavi na Njombe.
No comments:
Post a Comment