Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MBUNGE wa Viti maalum mkoani Ruvuma, Sikudhan Chikambo amezitaka
Halmashauri za wilaya mkoani humo kutekeleza jukumu la kupeleka asilimia 10 ya
fedha za mapato yake ya ndani katika vikundi vya ujasiriamali, kwa wanawake na
vijana.
Aidha amewaagiza madiwani wa mkoa huo, kuhakikisha kwamba
suala hilo wanalifuatilia kwa karibu ndani ya halmashauri zao kupitia vikao
husika, ili fedha hizo zielekezwe kwa kundi hilo.
Chikambo alitoa agizo hilo juzi, alipokuwa akizungumza na akina
mama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilaya ya Mbinga, katika kikao cha
baraza la wanawake kilichofanyika kwenye ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
mjini hapa.
Mbunge huyo alisema kuwa wanawake wanaweza kujituma kwa kila
jambo la kimaendeleo, hivyo wanapaswa wakati wote kutetea haki zao pale
wanapoona zinaporwa na watu wasiopenda maendeleo yao.
“Madiwani mliochaguliwa nawataka pia mrudi kwenye kata zenu
kutumikia wananchi na sio muda mwingi kuwa mbali, tuache sasa tabia ya
kutengeneza majungu na fitina tuunge mkono kauli mbiu ya Rais wetu John
Magufuli, ‘Hapa kazi tu’ kwa kufanya kazi kwa ushirikiano kwa maendeleo ya
taifa letu”, alisema Chikambo.
Vilevile aliwataka wanawake kujiunga katika vikundi vya
ujasiriamali, ili waweze kujikwamua katika maisha yao ya kila siku na sio muda
mwingi kulalamika na kukaa bila kujishughulisha katika kazi mbalimbali.
“Mimi binafsi nina ahidi kufanya kazi na wanawake wote wa
mkoa wa Ruvuma naomba nipeni ushirikiano, jukumu hili la ubunge mlilonipatia
linahitaji ushirikiano wa dhati, upendo na uaminifu ili tuweze kufikia malengo
ya kimaendeleo tuliyojiwekea”, alisisitiza Chikambo.
Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya UWT wilaya ya Mbinga,
Katibu wa umoja huo wilayani humo, Martina Katyale alisema kuwa wanachama
wamejiwekea mikakati ya kuimarisha miradi waliyonayo ya kimaendeleo ikiwemo
kuongeza upandaji wa miti ya mbao, kwa msimu wa mwaka 2016/2017 ngazi ya kata
na matawi.
Hata hivyo Katyale aliongeza kuwa katika kuendelea
kuimarisha mahusiano mazuri kwa wanachama wake, uongozi wa umoja wa wanawake
ngazi ya wilaya utafanya ziara ya kuwatembelea wanawake katika kata zote 48 kwa
lengo la kuhamasisha pia wajiunge katika vikundi vya ujasiriamali na kuhimiza
wanachama kulipa ada kwa wakati.
No comments:
Post a Comment