Dkt. Robert Elisha Mganga Mkuu hospitali ya Halmashauri mji wa Mbinga mkoani Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALI ya upatikanaji wa madawa kwa ajili ya kutibu wagonjwa
katika hospitali ya Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, imeelezwa kuwa
ni tatizo sugu ambalo linaendelea kuitesa jamii hivyo serikali imeombwa
kuingilia kati kutatua tatizo hilo ili wagonjwa wanaopata huduma katika
hospitali hiyo waweze kuondokana na kero hiyo.
Kadhalika imefafanuliwa kwamba upungufu huo wa madawa
unatokana na baadhi ya watumishi wa idara ya afya kutokuwa waaminifu, ambapo
inadaiwa kuwa dawa hizo wamekuwa wakiiba na kuziuza kupitia maduka yao ya dawa
muhimu yaliyopo mjini na vijijini huku wagonjwa wakilazimika kwenda kununua
kwenye maduka hayo.
Hayo yalisemwa katika kikao cha baraza la madiwani wa
halmashauri ya mji huo kilichofanyika juzi mjini hapa ambapo licha ya kuwepo
kwa changamoto hiyo, madiwani hao pia walilalamikia baadhi ya wauguzi kuwatolea
lugha mbaya wagonjwa ambao wanakwenda hospitalini hapo kupatiwa matibabu.
Pamoja na mambo mengine, diwani wa kata ya Mbinga mjini B
kupitia tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Emmanuel Widambe
alililamikia huduma ya jengo maalumu la kulaza wagonjwa daraja la kwanza (Grade
One) lililopo katika hospitali ya mji wa Mbinga, kwamba sio nzuri kutokana na
jengo hilo kujengwa chini ya kiwango ambapo nyakati za masika limekuwa likivuja
na kuleta adha kubwa kwa wagonjwa.
“Mheshimiwa Mwenyekiti jengo hili halifai kwa matumizi ya
wagonjwa, limekuwa likivuja hasa pale mvua zinaponyesha na pia miundombinu yake
ya ndani kama vile mfumo wa maji safi na salama, katika baadhi ya vyumba
imejengwa chini ya kiwango”, alisema Widambe.
Akijibu hoja hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji huo
Ndunguru Kipwele alifafanua kuwa katika msimu wa fedha wa mwaka 2016/2017
serikali itafanya ukarabati wa jengo hilo, huku akisisitiza kwamba suala la
upotevu wa madawa hospitalini hapo litafanyiwa kazi ili wahusika waweze
kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi.
No comments:
Post a Comment