Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge amesema kuwa hali
ya usafi katika Manispaa ya Songea mkoani humo, sio ya kuridhisha hivyo ameutaka
uongozi husika wa Manispaa hiyo kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo ili
isiweze kuleta madhara, ikiwemo magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.
Mji wa Songea. |
Dkt. Mahenge alisema hayo juzi kwenye kikao kilichohusisha
watumishi wa serikali, taasisi za umma, madiwani, wafanyabiashara na wazee ambacho
kilifanyika mjini hapa.
Alisema kuwa utunzaji wa mazingira na masuala ya usafi ni
jambo la lazima ambalo kila mwananchi, anapaswa kulitekeleza ili kuweza kuzuia
magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza na kuleta madhara katika jamii.
“Kampeni ya usafi katika mji wetu wa Songea ni jambo la
lazima kwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, agizo langu kwa Manispaa ondoeni
taka zote zilizopo kwenye maghuba’’, alisisitiza Dkt. Mahenge.
Mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa jukumu la kufanya usafi wa
mazingira ni endelevu na kwamba halmashauri zinapaswa kusimamia hilo kwa
kuhakikisha taka zote mkoani humo, zinakusanywa toka majumbani kwa wananchi na
kupelekwa sehemu maalumu kwa ajili ya kuziteketeza ili zisiweze kuleta madhara.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Songea,
Sekambo alitoa agizo kwa idara ya afya katika Manispaa hiyo kuhakikisha kwamba
wanashirikiana kwa pamoja katika kutekeleza jambo hilo, ili kuweza kufikia
malengo husika ya ukusanyaji wa taka zote zilizopo katika mji huo.
Sekambo alisema kuwa maeneo ya katikati ya mji wa Songea yanaridhisha
kwa usafi, isipokuwa katika maeneo ya pembezoni mwa mji huo ndiyo ambayo
yamekuwa machafu na watu wamekuwa wakitupa taka hovyo, ambapo alitoa rai kwamba
kwa atakayekamatwa atachukuliwa hatua za kisheria.
“Naagiza juhudi za kufanya usafi ziongezwe ili Manispaa yetu iweze
kuwa katika hali ya usafi, taasisi za shule na wafanyabiashara tushirikiane pia
kutekeleza jambo hili la usafi wa mazingira”, alisema Sekambo.
No comments:
Post a Comment