Na Julius Konala,
Songea.
ASKOFU Mkuu Josephat Lebulu wa kanisa Katoliki jimbo kuu la
Arusha amewapongeza masista wa Benedictine wa Afrika, shirika la mtakatifu
Agnes Chipole lenye makao yake makuu mjini Songea mkoani Ruvuma, kwa kutoa
msaada wa huduma mbalimbali kwa jamii.
Aidha imeelezwa kuwa wameweza kuanzisha mradi wa umeme wa
nguvu ya maji, ambao umesambazwa kwenye makazi ya watu kwa gharama nafuu.
Hayo yalisemwa na Askofu Lebulu alipokuwa akihubiri kwenye
ibada ya misa takatifu, Jubilei ya miaka 75 ya shirika hilo tangu kuanzishwa
kwake iliyofanyika katika viwanja vya nyumba ya malezi Chipole wilayani Songea.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali
wakiwemo maaskofu, wakuu wa mashirika ya kitawa, viongozi wa vyama vya siasa na
serikali.
Alisema kuwa katika kipindi chote cha miaka 75 tangu
kuanzishwa kwa shirika hilo wameweza kusaidia kutoa huduma mbalimbali za
kijamii, ambazo haziwezi kupimwa kwa rula au kufananishwa na kitu chochote.
Pia masista hao wamekuwa mstari wa mbele katika kupambana na
adui ujinga, maradhi na umasikini kwa kuanzisha shule za msingi, sekondari, vyuo,
zahanati pamoja na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mashine za kusaga
nafaka.
“Napenda kuwapongeza masista kwa malezi yenu ya kuwalea
watoto, vijana na wazee kwani kufanya hivi kunasaidia taifa kupata viongozi
waadilifu pamoja na miito mbalimbali katika kanisa ikiwemo upadre na utawa”, alisema
Lebulu.
Naye Askofu Mkuu Damian Dallu wa jimbo kuu Katoliki la Songea,
amewataka waumini hao kudumisha amani na kuheshimu imani ya mtu mwingine kwa
madai kwamba, taifa lolote linapoingia katika machafuko ya kivita shughuli
mbalimbali za kimaendeleo na kuabudu haziwezi kusonga mbele.
Kwa upande wake Mkuu wa shirika la masista wa Benedictine wa afrika
wa mtakatifu Agnes Chipole, sista Maria Hilalia mkalawa alipozungumza katika Jubilei
hiyo alisema kuwa shirika hilo tangu kuanzishwa kwake limeweza kupiga hatua
kimaendeleo, ikiwemo kuongeza idadi ya watawa hadi kufikia 773 ambapo kati yao
352 ni wa nyumba ya Chipole na 421 ni wa nyumba ya mtakatifu Getrudi Imiliwaa
Njombe na kwamba linahudumia katika majimbo 15 hapa nchini.
No comments:
Post a Comment