Waziri wa TAMISEMI George Simbachawene akisalimiana na watumishi halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, alipokuwa katika ziara yake ya kikazi hivi karibuni. |
Na Yeremias Ngerangera,
Songea.
WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene, amewataka watumishi wa umma ambao hawaendani
na kasi ya utendaji kazi wa serikali hii ya awamu ya tano, kwa hiari yao
wapishe ili nafasi hizo zichukuliwe na watu wengine.
Hayo yalisemwa na Waziri huyo wakati alipokuwa akizungumza hivi
karibuni na wakurugenzi na wakuu wa idara wa halmashauri za mkoa wa Ruvuma, kwenye
ukumbi wa Manispaa ya Songea mjini hapa.
Aidha Simbachawene alikemea watumishi hao akisema hakuna
sababu ya wao kuandamana kwa lengo la kudai haki zao, ikiwemo suala la kupandishwa
madaraja kwani hivi sasa mtumishi atapandishwa daraja kutokana na elimu yake
aliyonayo na uwezo wake wa utendaji kazi kiutumishi.
Simbachawene alifafanua kuwa mtumishi atakayeonekana kutotekeleza
vizuri majukumu yake, hatapandishwa cheo au daraja badala yake ataendelea
kubaki kama alivyo mpaka pale atakapofikia hatua ya kustaafu.
Pamoja na kutoa msimamo huo, Waziri huyo alipokea taarifa za maendeleo
kwa kila halmashauri iliyopo mkoani hapa ambapo pamoja na mambo mengine
aliwataka wakurugenzi, wakuu wa wilaya pamoja na wenyeviti wa halmashauri
kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba uchumi wa halmashauri zao unakuwa kwa
kasi ili wananchi waweze kuondokana na umaskini.
Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya mkoa huo Mkuu wa mkoa
wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge alisema kuwa mkoa wake una halmashauri nane
ambazo ni Mbinga mji, Mbinga vijijini, Tunduru, Nyasa, Madaba, Songea vijijini,
Songea Manispaa na halmashauri ya wilaya ya Namtumbo.
No comments:
Post a Comment