Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI wa kijiji cha Longa kata ya Mkumbi wilaya ya Mbinga
mkoa wa Ruvuma, wamelalamikia kitendo cha wizi wa kahawa zaidi ya magunia 100
ambao umefanyika kijijini humo na watu wasiojulikana.
Hali hiyo imeelezwa kwamba, kahawa iliyoibwa ni ile ambayo
ilianikwa kwenye vichanja nje ya ghala la kuhifadhia kahawa tayari kwa
kusafirishwa kwenda Kiwanda cha kukoboa kahawa Mbinga (MCCCO) kilichopo mjini
hapa.
Kufuatia tukio hilo walinzi wawili ambao walikuwa wakilinda
katika eneo la ghala la kuhifadhia kahawa hiyo, wanashikiliwa na mgambo katika
mahabusu ya kata hiyo wakidaiwa kuiba kahawa ambayo ilianikwa kwenye vichanja
hivyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti
wananchi hao ambao ni wakulima wa zao hilo, walisema kahawa yao imeibwa katika
mazingira ya kutatanisha majira ya usiku Agosti 11 mwaka huu.
Mwenyekiti wa chama cha ushirika Longa, Angelus Kimonile
aliwataja walinzi ambao wanawashikilia kuwa ni Jacob Komba na Anton Ndimbo
wakiwataka waeleze bayana juu ya wizi huo, uliofanyika kabla ya kuchukuliwa
hatua za kisheria za kuwafikisha mahakamani.
“Hawa walinzi tumewashikilia kwa lengo la kuwahoji na tunawataka
watueleze mpaka wizi huu unafanyika wao walikuwa wapi, tunamashaka nao huenda
wao ndio waliocheza mchezo huu mchafu”, alisema Kimonile.
Pia aliongeza kuwa tukio hilo linahusishwa na mgogoro
uliodumu kwa muda mrefu kwa baadhi ya wanachama wa ushirika huo, kuwakataa
viongozi waliopo madarakani wakiwataka waondoke na uchaguzi ufanyike upya
kuwachagua wengine.
Alisema kuwa mgogoro huo umedumu kwa miaka miaka miwili ambapo
wanachama wanataka uundwe uongozi mpya, kutokana na uliopo sasa kutokuwa na
imani nao jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Gombo
Samandito aliwaambia waandishi wa habari kwamba kufuatia tukio hilo ameunda
timu ya kufuatilia suala hilo, ili liweze kufikishwa kwenye vyombo vya
kisheria.
No comments:
Post a Comment