Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI wa kijiji cha Ilela kata ya Mikalanga wilayani
Mbinga mkoa wa Ruvuma wamesema kwamba ipo siku wataandamana kuelekea ofisi ya
Mkuu wa wilaya hiyo, kwa lengo la kuiomba serikali kuingilia kati mgogoro ambao
umedumu kwa muda mrefu sasa kati yao na taasisi ya Ansary Muslim Youth Center, iliyopo
mjini hapa ambayo inadaiwa kupora jengo lao la biashara.
Jengo hilo ambalo ni maarufu kwa jina la Ilela, ni kitega
uchumi ambacho kilijengwa na wananchi hao mwaka 1980 kwa lengo la kupangisha
wafanyabiashara wa aina mbalimbali, ili waweze kujipatia fedha kwa ajili ya
kufanyia maendeleo yao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa kijiji
hicho Anton Komba alisema kuwa mgogoro huo umekuwa ukiwakera kutokana na kudumu
kwa zaidi ya miaka 15 na hakuna mafanikio, hivyo wanaiomba serikali iwasaidie
ili waweze kunusuru jengo lao.
Komba alisema kuwa licha ya suala hilo kufikishwa kwa
viongozi wa ngazi ya wilaya hakuna mafanikio yanayoonesha kuzaa matunda juu ya
tatizo hilo.
Alisema kuwa taasisi ya Muslim Youth Center imejiuzia jengo
hilo kwa shilingi milioni 5 kupitia aliyekuwa mpangaji ambaye anafahamika kwa
jina la Yordan Konzo bila kufuata taratibu husika.
Kadhalika alibainisha kuwa Konzo alifanya tukio hilo la kupiga
mnada jengo hilo na kuliuza kwa fedha hizo, akidai kwamba uongozi wa kijiji cha
Ilela alikuwa anaudai shilingi 900,000 jambo ambalo sio la kweli.
“Wamiliki wa jengo hili ni wananchi wenyewe na hata tukifanya
leo hii uthaminishaji wa jengo hili mali zilizopo pale ni zaidi ya milioni 800,
inakuwaje yeye apige mnada na kuliuza kwa shilingi milioni tano?”, alihoji
Komba.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa suala hilo ambalo lipo pia
mezani kwa viongozi wa wilaya ya Mbinga, utekelezaji wake umekuwa ukisuasua hivyo
wanajipanga kwenda kumuona Mkuu wa wilaya hiyo ili jengo lao libakie mikononi
mwa wananchi.
Vilevile mwandishi wa habari hizi alipofanya mahojiano na Yordan
Konzo ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya jambo hilo, alisema yeye alifuata
taratibu husika wakati anapiga mnada jengo hilo ili aweze kupata fedha zake
anazokidai kijiji hicho.
Hata hivyo Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye alisema
kwamba jambo hilo atalifanyia kazi ili kuweza kumaliza mgogoro huo usiweze
kuendelea na mali za wananchi hao, zibakie katika mikono yao kama ilivyokuwa
hapo awali.
No comments:
Post a Comment