Tuesday, August 16, 2016

TUNDURU WALIA NA TEMBO WANAOVURUGA MAZAO YAO KAYA 2,000 ZIPO HATARINI KUKUMBWA NA NJAA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge.


Na Steven Augustino,      
Tunduru.

ZAIDI ya kaya 2,000 zinazoishi katika vijiji vilivyopo kata ya Kalulu na Mbungulaji wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wapo hatarini kukumbwa na baa la njaa kutokana na mazao yao waliyolima shambani kushambuliwa na kuvurugwa na kundi la tembo waliojitokeza kutoka hifadhi ya taifa ya Selous.

Taarifa ya tukio hilo ilitolewa na Salum Bakari, Alli Amani na Abdalla Kindimba ambao ni wakazi wa maeneo hayo ambapo walimweleza hayo Mkuu wa wilaya hiyo, Juma Homera alipowatembelea kwenda kujionea juu ya uharibifu huo uliofanyika.

Wananchi hao waliendelea kusema kuwa hivi sasa wanaishi kwa hofu baada ya mazao yao ya mpunga, mahindi, migomba ya ndizi, maharage, ufuta, mihogo na vitunguu kushambuliwa na wanyama hao na kuwafanya waishi katika mazingira magumu.


Walidai kuwa pamoja na kuwepo kwa baadhi ya wananchi ambao wakati mwingine wamekuwa wakipata madhara yatokanyo na tembo hao, lakini wafanyakazi wa idara ya wanyama pori wamekuwa wakiwatolea lugha chafu hasa pale wanapokwenda kudai fidia husika.

Aidha katika malalamiko hayo wananchi hao waliwatuhumu waziwazi mbele ya Mkuu huyo wa wilaya ya Tunduru, askari wanaoishi katika kambi ya Kalulu kwamba wamekuwa wazembe katika majukumu yao hususani kuwafukuza tembo hao ili wasiweze kuendelea kuleta madhara kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.

Walisema mpaka sasa tayari watu watatu wameuawa kutokana na wanyama hao kuzurula hovyo mitaani kama mbuzi na kwamba, mpaka sasa hakuna familia iliyopewa pole au kulipwa fidia kutokana na madhara hayo yaliyojitokeza.

Akizungumzia juu malalamiko hayo mkuu wa kanda ya Kalulu, Issack Mwamshi alisema kuwa sera, kanuni na sheria za kazi za uhifadhi hapa Tanzania haziwaruhusu kuua wanyama hao bali wanatakiwa kuwafukuza na kuwarejesha katika makazi yao.

Naye Kaimu afisa wanyama pori wilaya ya Tunduru, Peter Mtani alikiri kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazao ya wakulima katika vijiji vya kata za Kalulu na Mbungulaji.

Alisema pamoja na uwepo wa takwimu za sensa iliyofanyika mwaka 2014 walibaini uwepo wa jumla ya tembo 15,000 lakini idara yake, inakabiliwa na changamoto kubwa ya kupungua kwa tembo hao na kwamba tangu nchi ipate uhuru imepoteza asilimia 90 ya tembo wake.

Kwa upande wake akijibu kero za wananchi hao Mkuu wa wilaya hiyo, Homera aliwataka wananchi hao kuwa watulivu akisema kuwa serikali inandaa utaratibu wa kuwalipa fidia wananchi wote waliopata madhara hayo pamoja na kufanya utafiti wa chanzo cha wanyama hao, juu ya kuhama katika makazi yao na kuingia katika mashamba ya watu.

Hata hivyo alimtaka afisa wanyamapori wa wilaya hiyo, Mtani kuandaa taarifa ya upungufu wa chakula katika vijiji hivyo na kuipeleka ofisini kwake mapema, ili kuweza kuandaa utaratibu wa kuwapelekea chakula kingine wananchi hao wasiweze kuteseka na njaa.

No comments: