Wednesday, August 31, 2016

WAHAMIAJI HARAMU WAKAMATWA GUMBIRO SONGEA WAKITOKEA DAR ES SALAAM



Na Mwandishi wetu,           
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na Maofisa wa idara ya uhamiaji wamefanikiwa kuwatia mbaroni watu watatu ambao ni raia wa nchi ya Ethiopia wakiwa ndani ya basi la Super Feo, wakitokea Jijini Dar es Salaam kuelekea nchi ya Msumbiji kupitia Songea mkoani hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 23 mwaka huu katika kijiji cha Gumbiro wilaya ya Madaba mkoani humo.

Mwombeji aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Halima Said Bachu (27) mkazi wa Oromo Ethiopia ambaye alikuwa anajishughulisha na shughuli za kibiashara huko Jijini Nairobi nchini Kenya.


Kadhalika alimtaja mwingine kuwa ni Etwayo Baurehiman (25) na Etharse Mohamed (27) ambao ni wanafunzi wa chuo kikuu cha Asasa kilichopo Omoro Ethiopia.

Alifafanua kuwa raia hao wa Ethiopia, wanadaiwa kuingia hapa nchini bila kibali maalum wakiwa na lengo la kuelekea nchi ya Afrika Kusini kupitia Msumbiji, kwenda kutafuta maisha bora.

Hata hivyo walikamatwa wakiwa ndani ya basi linalosafirisha abiria, Kampuni ya Super Feo lenye namba za usajili T 587 DFT aina ya Higue lililokuwa likitokea Dar es Salaam, kuelekea Songea na kwamba watuhumiwa hao wapo chini ya ulinzi mkali na wamekabidhiwa kwenye idara ya uhamiaji mkoani Ruvuma kwa hatua zaidi za kisheria.

No comments: