Rais Dkt. John Magufuli. |
Na Julius Konala,
Songea.
BAADHI ya wananchi wa kata ya Mwengemshindo Manispaa ya
Songea mkoani Ruvuma ambao maeneo yao yametwaliwa na shirika la EPZA kwa
kipindi cha miaka tisa iliyopita bila kuwalipa fidia yoyote, wamemuomba Waziri
wa viwanda na biashara, Charles Mwijage kuingilia kati suala hilo ili waweze
kupata haki yao ya msingi.
Ombi hilo lilitolewa juzi na wananchi hao mbele ya Mbunge
wa jimbo la Songea mjini Leonidas Gama, katika mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye uwanja wa michezo wa kata hiyo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa
siasa na serikali.
Walisema kuwa tangu maeneo yao yachukuliwe wamekuwa
wakiishi katika maisha magumu kutokana na kuzuiwa kuendesha shughuli yoyote ile,
ikiwemo kilimo cha mazao ya chakula na biashara ili waweze kujipatia kipato
katika maisha yao ya kila siku.
Akizungumza katika mkutano huo mmoja kati ya wakazi wa
eneo hilo, Otmary Komba alisema kuwa kutokana na kucheleweshwa kulipwa fidia ya
maeneo yao baadhi yao, wanashindwa hata kusomesha watoto wao shule huku familia
zikikosa pia mahali pa kuishi.
Kwa upande wake Mbunge huyo aliwataka wananchi hao kuwa
watulivu wakati serikali inaendelea kushughulikia suala hilo, na akaongeza kwamba
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekwisha pitisha bajeti kwa ajili ya
fidia ya maeneo yao.
Gama alisema kuwa eneo hilo lenye ukubwa usiopungua
ekari 5,000 litakuwa pekee kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda mbalimbali, hivyo
amewataka wazazi kusomesha vijana wao ili waweze kunufaika na ajira pindi
viwanda hivyo vitakapoanza kufanya kazi.
“Ndugu zangu sitaweza kuzungumzia kwa kina juu ya suala
la baadhi ya wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa na EPZA kwa kuwa shauri
hilo lipo Mahakamani linashughulikiwa kisheria, siruhusiwi kulizungumzia hapa
mpaka mchakato wake utakapokuwa umekwisha”, alisema Gama.
No comments:
Post a Comment