Sixtus Mapunda, Mbunge wa jimbo la Mbinga mjini akisisitiza jambo katika kikao alichoketi jana wakati akizungumza na watumishi wa idara ya afya katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WATUMISHI wa idara ya afya hospitali ya Halmashauri ya mji wa
Mbinga mkoani Ruvuma, wameutaka uongozi wa halmashauri hiyo kuwalipa madai yao
ya aina mbalimbali ili waweze kutatua matatizo yao yanayowakabili katika maisha
yao ya kila siku.
Watumishi hao wakichangia hoja mbalimbali. |
Madai hayo walifafanua kuwa ni malimbikizo ya fedha za
likizo, matibabu na safari ambapo hawajalipwa kwa muda mrefu sasa na hawajui hatima
yake kwa kile walichoeleza kuwa wamekuwa wakifuatilia mara kwa mara, kwa
uongozi husika na hakuna dalili zinazoonesha kuzaa matunda.
Hayo yalisemwa jana na watumishi hao walipokuwa wakizungumza
na Mbunge wa jimbo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda ambaye aliwatembelea
hospitalini hapo kwa lengo la kusikiliza na kupokea kero zao za aina mbalimbali
ili ziweze kufanyiwa kazi.
Raymond Ngatunga ambaye naye ni muuguzi wa hospitali hiyo
alieleza kuwa yeye na watumishi wenzake wamekuwa wakidai madai hayo kwa muda
mrefu, hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuona umuhimu wa kutekeleza jambo
hilo mapema ili waweze kuondokana na mazingira magumu katika kusukuma mbele
maisha yao.
Kadhalika baadhi yao walilalamikia suala la kutothibitishwa
kazini, licha ya kwamba wamefanya kazi hospitalini hapo kwa muda mrefu.
Akitolea majibu juu ya madai hayo kwa niaba ya Mbunge huyo,
Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dkt. Elisha Robert alikiri juu ya watumishi hao
kudai madai hayo na wengine kutothibitishwa kazini ambapo halmashauri inafanya
jitihada ya kumaliza kero hiyo ikiwemo kulipa madeni hayo.
“Mheshimiwa Mbunge, hata hospitali pia imekuwa ikidaiwa bili
za maji na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira bado hayajalipwa kwa muda
mrefu, tunaomba wawe wavumilivu tutawalipa kulingana na kiasi cha fedha
tutakachoanza kupokea kutoka serikalini”, alisema Dkt. Robert.
Kwa upande wake Mbunge, Mapunda alisisitiza kwa kuutaka
uongozi husika katika halmashauri ya mji wa Mbinga kuhakikisha kwamba madai ya
watumishi hao yanalipwa kwa wakati ikiwemo pia suala la kuwathibitisha kazini,
ili waweze kufanya kazi kwa moyo wa kujituma na sio kuwa na manung’uniko
yasiyokuwa na kikomo.
“Hawa watu wanataka haki zao, mtu anayedai deni lake ni
lazima ulipe hivyo nasisitiza kwa mamlaka husika kulifanyia kazi tatizo hili
haraka, ili tuweze kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima”, alisema Mapunda.
Pamoja na mambo mengine Mbunge huyo aliwataka watumishi wa
idara ya afya katika hospitali hiyo kujenga ushirikiano, kuwa wazi wakati wote katika
utendaji wao wa kazi na kuacha majungu.
No comments:
Post a Comment